NA HAFSA GOLO
IDARA ya Uhamiaji Zanzibar imesitishwa kuendelea na ujenzi wa vibanda vipya vya kupokelea wageni wanaoingia nchini katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Abeid Amani Karume.
Hatua hiyo imekuja baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo kutoridhishwa na kiwango cha fedha kinachotarajiwa kutumika katika ujenzi huo na kusitisha zoezi hilo mara moja.
Naibu waziri huyo aliyefanya ziara kwenye taasisi zilizo chini ya wizara yake zilizopo Zanzibar, alisema shilingi milioni 64 zilizopangwa kutumika katika mradi huo ni nyingi hivyo aliagiza viongozi wakae tena chini kupitia upya mikataba iliyofungwa.
“Hatukuwekwa viongozi kwa ajili ya kuzuia miradi, ila kazi yetu ni kuhakikisha fedha za miradi ya serikali zinatumika vyema na sio watu wengine wanatia mifukoni mwao”, alisema.
Naibu huyo, alisema lazima watendaji wawe makini katika matumizi ya fedha za serikali hasa ikizingatiwa yapo mahitaji mengine muhimu yanayohitaji kufanyika kwa ajili ya maendeleo.
“Kiwango cha fedha kinachotaka kutumika katika ujenzi huu kimenitia mashaka kutokana na uhalisia wa kazi yenyewe ilivyo”, alisema.
Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa tatizo la msongomano wa upatikanaji wa huduma katika kiwanja hicho na kuahidi kuifanyia kazi changamoto hiyo kwa kipindi kifupi suala hilo ili wananchi waondokane na tatizo hilo.
Alisema zoezi la ujenzi litaendelea baada ya kuhakikisha fedha zitakazotumika zitaendana na mahitaji yalivyo.
Wakati huo huo katika ziara hiyo naibu huyo hakuridhika na matumizi ya fedha ya zaidi ya shilingi milioni 500 zilizotumika kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za wafanyakazi wa Idara hiyo zilizojengwa Kiembesamaki Unguja.
Aliagiza kupatiwa nyaraka zote za mkataba zilizotumika katika ukarabati wa nyumba hizo na ziambatanishwe na ripoti ya ukaguzi zilizofanyika katika ukarabati huo.
Alisema iwapo atabaini kuna udanganyifu umefanyika katika ukarabati huo hatua za sheria zitachukua nafasi yake kwa wahusika.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya wananchi juu ya upatikanaji wa hati ya kusafiria kwa wakati, alisema tatizo hilo alibaini katika ziara hiyo linachangiwa na wananchi wenyewe kwa sababu ya kutokamilisha taratibu zinazohitajika.
Hata hivyo, aliishauri idara hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuwa na uelewa kwa kutimiza masharti na taratibu wakati wanapohitaji maombi ya hati hizo.
Naye Mratibu Mwandamizi wa Uhamiaji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Bakari Mohamed Ameir, alisema chanzo kinachochangia kuwepo kwa msongomano wa abiria ni pamoja na idadi ya ndege za kimataifa zinazoingia nchini kuongezeka.
Alifahamisha kwamba Disemba 19 kiwanjani hapo ziliingia ndege za Kimataifa 10 kuanzia saa 12:43 hadi saa 11 jioni.