NAMARYAM HASSAN

NAIBU waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Hamza Khamis, amesema atahakikisha anatumia sheria na kanuni zinazowaongoza katika kuvifanyia kazi vikwazo vinavyosababisha kuendelea kuwepo tatizo la dawa za kulevya na rushwa.

Akizungumza na maofisa wa vitengo mbali mbali vya Jeshi la Polisi Makao Makuu ya jeshi hilo Zanzibar, alisema kuendelea kuwepo kwa hali hiyo kumekuwa kukiathiri jamii na kuharibu sifa ya jeshi hilo lenye dhamana na kulinda usalama wa raia na mali zao.

Alisema kumekuwepo kwa baadhi ya watumishi wa jeshi hilo wasiokuwa waaminifu ambao wanakiuka maadili ya kazi zao kwa kujihusisha na vitendo hivyo na kukwamisha mambo ambapo inahitaji nguvu ya pamoja katika kuviondoa na kufikia lengo la raia kuwa na imani na utendaji wa jeshi hilo.

Akizungumzia miradi ya jeshi hilo yaliyosua kipindi kirefu, ikiwemo ujenzi wa nyumba za makaazi na vituo visivyokuwa rasmi ambapo utekelezaji wake umekuwa hauridhishi, alisema kuwa atahakikisha ufafanuzi unatolewa kwa waliokabidhiwa ili kuweza kujulikana kitu gani kilichokwamisha miradi hiyo.

Hivyo alisema katika uongozi wake atahakikisha anavifanyia kazi ili kujua sababu zilizopelekea kutokutekelezwa kwa miradi hiyo kukwama hadi sasa ukizingatia fedha zimetolewa na serikali.

“Fedha za wananchi ndio zinazotumika ila cha kushangaza hadi sasa miradi hiyo haijamaliza ikiwemo nyumba za polisi bububu pamoja na nyumba za askari”, alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa kumekuwepo kwa changamoto za polisi zinazowakabili na kuahidi kuzichukua na kwenda kuzifanyia kazi ili kuweza kufanya kazi katika mazingira yaliyokuwa bora.