NA HUSNA SHEHA

MAHAKAMA ya Wilaya Mahonda, imempeleka Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwaka mmoja na nusu Hamad Rajab Mmanga (25) mkaazi wa Donge camp Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, kwa kosa la wizi wa mazao.

Hakimu wa Mahakama hiyo Nyange Makame Ali, alitoa adhabu hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Mashitaka na kumuona mshitakiwa kuwa ni mkosa wa kosa hilo, na mahakama ikamtia hatiani.

Mshitakiwa huyo alipelekwa chuoni kwa kosa la wizi wa mazao, kitendo ambacho ni kosa kinyume na kifungu cha sheria namba 251 (1) na 268 (1) (2) (3) vya sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Kabla ya hukumu hiyo, upande wa mashitaka uliokua ukiongozwa na Wakili wa serikali, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Suleiman Khamis, alieleza kuwa hauna kumbu kumbu za makosa mengine kwa mshitakiwa huyo, huku akiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ya familia yake masikini.

Mbali ya hukumu hiyo, pia ametakiwa kulipa fidia fedha shilingi 1,400 ikiwa 52,000 za mlalamikaji na 52,000 za serikali, na endapo akishindwa ataongezwa miezi mitatu yakutumikia chuoni.

Mshitakiwa huyo aliiba nazi 8 zenye thamani ya shilingi 5,600 kwa makisio, ikiwa ni mali ya Ame Machano Bakari, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Alidaiwa kufanya wizi huo Agosti 5 mwaka huu majira ya saa 1:00 usiku katika kijiji cha Donge Camp Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.