KIJA  ELIAS, ROMBO

NCHI za Afrika Mashariki, zilizoingia makubaliano ya soko la pamoja zimetakiwa kurejea kwenye makubaliano yao ya awali, ili kuleta mifumo rasmi zitakazo wavutia wafanyabiashara kutaka kufanya biashara zaidi katika maeneo hayo.

Hayo yamebainishwa juzi na Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama kutoka Sekta binafsi TPSF), Zachy Mbena, wakati alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wadogo, wasafirishaji  pamoja na  maofisa wa forodha katika mpaka wa Taveta uliopo wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro.

Alisema wafanya biashara wanapopeleka biashara zao katika nchi ya Kenya wamekuwa wakikumbana na vikwazo mbalimbali  ambavyo vinakwamisha maendeleo ya kiuchumi na hivyo kuwasababishia kutumia muda mrefu.

Alisema vikwazo hivyo vinatokana na watumishi  wanaofanya kazi katika mipaka hiyo  na hivyo kusababisha wafanyabiashara kutafuta namna ya kukwepa kwa kupita njia zisizo rasmi.

“Tunazitaka nchi za Afrika Mashariki kurejea katika makubaliano waliyoyasaini ya kufanya kazi pamoja, ili kuleta mifumo rasmi zitakazo wavutia wafanyabiashara kutaka kufanya biashara zaidi,” alisema.

Aidha alizitaka kamati zinazosimamia meza za biashara katika nchi za Afrika Mashariki zikutane mara kwa mara, ili kujadili vikwazo na changamoto zilizopo kwenye mipaka.

“Tunataka kuboresha mazingira ya biashara kwa kuwezesha biashara kwenye sehemu za mipaka, ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa nchi,” alifafanua.

Nae Ofisa Biashara Mkuu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Aneth Simwela, alizitaka taasisi ambazo zinahusika kutoa huduma kwenye mipaka kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi ili kupunguza vikwazo vya biashara ya ushuru.

“Watumishi hawa endapo wataendelea kuwa vikwazo, wafanyabiashara hawatapenda kupita katika mipaka halisi iliyowekwa na badala yake wataendelea kupita kwenye njia za panya ambazo siyo rasmi na hivyo watapunguza biashara na kukosa takwimu halisi za biashara zinazopita katika mipaka yetu,” alisema Simwela.

Aliongeza “Niwatake watumishi wa mipakani tujitahidi sisi tusiwe sehemu ya vikwazo na kusababisha Serikali kukosa mapato,” .

Awali wakizungumza baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia mpaka wa Tarakea, walisema utekelezaji wa mkataba ambao Tanzania imeusaini wa urahisishaji wa biashara bado nchi za Afrika Mashariki hazijaufuata kikamilifu.

Hassan Amed mfanyabiashara wa mazao ya misitu, alisema mazingira ya ufanyaji biashara kwa upande wa Tanzania ni mazuri, ila unapofika upande wa Kenya kunakuwa na vikwazo vingi.

“Unapofika na mzigo wako  upande wa Kenya, kwenye ukaguzi ambao unatakiwa ufanyike kwa muda mfupi huko hawafanyi hivyo unakaa hapo kwa siku tatu hadi tano, hali ambao inasababisha kukosa soko kutokana na ucheleweshwaji huo,”.

Alifafanua kuwa “Kila nikipeleka mzigo wangu natakiwa kukata kibali, nilikuwa ninaomba niruhusiwe kutengeneza kibali cha muda mrefu ambacho kitaniwezesha kila ninapopeleka mzigo wangu niweze kuruhusiwa kupita bila vikwazo,”.

” Tunamshukuru sana Rais Dk. Magufuli kuwa kutuunganisha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwa kitu kimoja kwenye masuala ya biashara,” alisema Amed.

Baraka  Mwaikuga ambaye ni msafirishaji, alisema changamoto zipo kwa upande wa Kenya, unakubaliana na mteja usafirishe mzigo wake kupeleka Nairobi, unapofika upande wa Kenya unaanza kucheleweshwa na wahusika wa forodha.

Naye Amedeus Mzee kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema ili kurahusisha mazingira ya kibiashara  ni vema taasisi zinazofanya shughuli za forodha kwenye mipaka zikapunguza vikwazo ili kurahisisha muda wa kukaa kwenye mipaka.

Alisema kuwa ni lazima Serikali kuyajua matatizo wanayokumbana nayo wafanyabiashara na kuyafanyia kazi ili wananchi wanufaike na fursa zilizopo katika mazingira yao, huku akiwataka watumishi wa Idara zote za Serikali zinazotoa huduma katika mipaka kutokuwa kikwazo kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara katika mpaka huo bali wawe wabunifu katika kazi zao.

“Sisi watumishi wa umma tusiwe kikwazo kwa watu wetu, kuwa mpakani ni fursa kubwa ya wananchi wetu kutajirika, ukienda nchi nyingine wananchi wa mipakani ndiyo matajiri kwa sababu wamepewa fursa ya kufanya biashara katika pande zote mbili lakini kwa kuzingatia matakwa ya sheria,”alisema