KAMPUNI moja ya Israel imesema ndege isiyokuwa na rubani, ambayo ilikamilisha safari yake ya kwanza kabisa ikipaa juu ya maeneo tambarare mwezi Novemba, huenda ikaanza kutumika rasmi kusafirisha abiria.

Ndege hiyo imeundwa na kufanyiwa kazi kwa kipindi cha miaka 15, lengo likiwa kutumika katika juhudi za uokoaji au shughuli za kijeshi.

Ndege hiyo ambayo inafahamika kama Cormorant iligharimu dola milioni 14 na inaweza kubeba mizigo ya uzani wa kilo 500 na kwenda kwa kasi ya kilomita 185 kwa saa.

Kampuni ya Urban Aeronautics imesema ndege hiyo ina rafadha (mapanga yanayozunguka kwa kasi ili kuendesha chombo) zilizo ndani na hilo linaifanya kuwa salama zaidi kushinda helikopta.

Kandi na kuweza kupaa juu na kutua bila kuhitajika kusonga mbele au nyuma, inaweza kupaa kupitia kati ya majumba na hata kupitia chini ya nyaya za umeme.

Hivi karibuni kamapuni ya Amazon ilitangaza kuanzishwa kwa huduma ya Prime Air, ambapo ndege zisizo na rubani zinatumiwa kusafirisha bidhaa kwa wateja.

Aidha mnamo mwezi Juni mwaka huu, ndege nyingine isiyo na rubani ambayo ilitengenezwa na kampuni ya Ehang kutoka China ilipewa idhini ya kufanyiwa majaribio huko katika jimbo la Nevada nchini Marekani.

Mtaalamu wa ndege zisizo na rubani Ravi Vaidyanathan, alisema mafanikio ya safari ya majaribio ya ndege hiyo ya Israel ni ufanisi mkubwa na kwamba ni uamuzi wa busara kwanza kuitumia kwa juhudi za uokoaji na shughuli za kijeshi.

Lakini ingawa huenda muda mfupi baadaye zikatumiwa kwa safari za kiraia na kusaidia kufika hasa maeneo yasiyo na miundombinu au yenye misongamano ya gari bado ni mapema kujua hilo litatekelezwa kikamilifu linu.

“Kuna changamoto nyingi za kihesheria, mfano kuhusu ni wapi unaruhusiwa kupaa? Ni wapi unaweza kutua? Unaruhusiwa kupaa juu hadi wapi?” alisema.