NA ABOUD MAHMOUD

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema mwezi Januari mwaka 2021, itazifungia jumuiya zote zisizo za Kiserikali ambazo haziwajibiki na hazioneshi uhai na kufanya kazi kwa mujibu wa katiba zao .

Hayo yamesemwa na Mrajis wa Jumuiya Zisizo za Kiserikali Zanzibar, Ahmed Khalid Abdulla, alipokutana na Zanzibarleo huko ofisini kwake Vuga mjini Unguja na kueleza kwa kina kuhusu mpango wao huo.

Mrajis huyo, alisema mpango huo unatokana na lengo la kufanya uhakiki wa kuzitambua jumuiya zote zisizo za kiserikali nchini na kufanya maamuzi yanayofaa ikiwemo kuziondoa kwenye usajili wa jumiya ambazo hazifanyi kazi.

“Tunatarajia mwezi Januari mwakani NGO’s zote ambazo haziwajibiki inavyotakiwa ikiwemo kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ya katiba zao tutazifutia usajili na kuzifungia,”alisema.

Mrajis huyo alieleza kwamba baada ya kukamilika kwa sheria inayohusu jumuiya hizo zisizo za kiserikali mafanikio yatakayopatikana ni kuundwa kwa baraza na  bodi za NGO’s ambapo zitasaidia kutoka fursa kwa taasisi hizo kuzungumzia changamoto mbali mbali zinazowakabili ili kuzifikisha Serikalini .

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuzidisha kujenga mashirikiano ya karibu zaidi  kati ya NGO’s hizo na SMZ katika kuleta maendeleo ya nchi na taasisi hizo kwa ujumla.

Alieleza kwamba kwa kipindi kirefu NGO’s zilikua na kilio cha kutaka marekebisho ya sheria nambari 6 ya mwaka 1995 ambapo Serikali imechukua juhudi za makusudi kuanza kulifanyia kazi suala hilo na kupitia rasimu ya sheria kwa kukusanya maoni ya wanajumuiya hizo katika Mikoa mitano ya Unguja na Pemba.

Ahmed alifahamisha kwamba NGO’s visiwani humu zimeanza kuwajibika na kufanya kazi kwa maendeleo ya jamii kwa kutoa mashirikiano endelevu kati yao na SMZ .

Alifahamisha kwamba iwapo juhudi hizo zitaendelea katika kipindi kifupi kijacho mabadiliko makubwa yatapatikana yanayotokana na NGO’s katika kuleta maendeleo ya nchi.