NA NASRA MANZI
BENKI ya NMB tawi la Zanzibar imetoa shilingi milioni 25 kwa ajili ya mshindi wa kwanza na wa pili wa mashindano ya kombe la Mapinduzi, inayotarajiwa kuanza Januari 5 katika uwanja wa Amaan.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo pamoja na fedha, Meneja Msimamizi wa Biashara tawi la Zanzibar Abdalla Duchi,alisema wanaimani kuwa fedha hizo zitasaidia kufanikisha mashindano hayo.
Aidha Meneja alikabidhi nguo za mazoezi 60 kwa ajili ya siku ya mazoezi Junuari 1, ambayo yataanzia kiwanja cha Mapinduzi Square Mnarani, kupitia barabara ya Biziredi na kumalizikia uwanja wa Amaan.
Alisema michezo ina fursa nyingi Zanzibar kwani wachezaji wengi wanaotoka Zanzibar wanacheza katika ligi kuu Tanzania Bara, jambo ambalo linaonesha kuwa Zanzibar inaendelea kukuza vipaji kwa vijana.
Hata hivyo alisema NMB ipo tayari kushirikiana na jamii ili kuona Zanzibar inaibua vipaji vingi pamoja na kwenda na kasi na muelekeo wa awamu ya nane ili kuimarisha michezo.
Nae Waziri wa wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alisema watashirikiana na NMB katika kufanikisha ligi ya Zanzibar kwani bado wana safari ndefu ya kuhakikisha michezo inapiga hatua visiwani.
Aliwashukuru NMB kwa kuthamini michezo Zanzibar kwani italeta mafanikio katika kuhakikisha vipaji vinazidi kupatikana na viwango vya wachezaji nchini.