MZEE GEORGE
MKUU wa mkoa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa ameliagiza jeshi la polisi mkoani humo, kumkamata ndugu Abubakar Mwinyi Hassan, kwa kudharau wito wa Mkuu wa mkoa huyo uliolenga kutatua mgogoro wa ardhi.

Kitwana alitoa agizo hilo Mwera Minanasini, shehia ya Mwembe Mchomeke baada ya mwananchi huyo kutofika katika kikao cha kuupatia ufumbuzi mgogoro wa ardhi kati yake na wananchi wengine akiwemo Mustafa Jaffar aliyekuwa akiihudumia eka hiyo.

Kitwana alisema, alizungumza na mwananchi huyo siku moja kabla na kumtaka afike katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Riziki Pembe Juma na uongozi wa wilaya ya Magharibi ‘A’.

“Nilimwita kufuatia malalamiko ya wananchi wa eneo hili kudai kupokea vitisho, kutozwa fedha, bughudha na hadi kufikia kuvunjiwa nyumba jambo ambalo lilihitaji kupata maelezo ya pande zote mbili,” alisema kitwana.

Alisema kitendo cha kutofika kwake katika kikao hicho sio dharau tu, bali kinaonesha mwananchi huyo ni mkorofi hivyo anapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Kutofika hapa kunaonesha ni jinsi gani anavyoweza kudharau mamlaka na hatua yake ya kuvunja nyumba na kuwabughudhi wananchi wenzake, inaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani na kuharibu ustawi wa jamii jambo ambalo halivumiliki,” alisema Kitwana.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Pembe, aliagiza kufutwa kwa hati ya umiliki wa eka aliyonayo Aboubakar na kurudishwa serikalini pamoja na kusitishwa kwa shughuli zote katika eneo hilo.

“Kwa mamlaka niliyonayo, nafuta hati ya heka hii kwani inaonekena imetolewa bila ya kufuatwa taratibu, viongozi wa serikali ya wilaya nakuombeni msimamie hili agizo kwa kuhakikisha kuwa hakuna shughuli yeyote inayofanyika hapa,” alieleza Pembe.

Aidha aliitaka serikali ya mkoa huo kushirikiana na serikali ya wilaya kuendelea kufuatia mgogoro huo na kuhakikisha wananchi wenye makaazi na wanaolima katika eka hilo hawabughudhiwi na wanapatiwa haki zao.

Alisema amechukua hatua hiyo baada ya kubaini ukiukwaji mkubwa wa sheria na matumizi bora ya ardhi za eka kwa kuuzwa viwanja na ujenzi wa nyumba za makaazi jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa matumizi ya eka.

Wakati huohuo waziri huyo ameitaka serikali ya mkoa Mjini Magharibi, kuzikusanya hati zote za umiliki wa eka zilizotolewa miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu uliopita kufuatia kuwepo kwa malalamiko ya kudhulumiwa eka inayoshughulikiwa na Haji Hassan Vuai na Khadija Burhan Ame wakaazi wa shehia hiyo.

“Na katika kesi hii, inaonekana pia kuna uonevu mkubwa hapa. Wananchi wetu hawa wanyonge wanadhulumiwa ardhi zao, hivyo agizo tulilolitoa la kufuta hati za umiliki wa eka zilizotolewa miezi miwili kabla ya uchaguzi, linatumika hapa pia,” alisema Waziri huyo.

Wakizungumza katika ziara ya viongozi hao, baadhi ya wanachi wanaoishi katika eka ya abubakar walisema wamekuwa wakipata vitisho na hatua ya kuvunjiwa nyumba zao.

“Tunaishi kwa wasiwasi toka huyu bwana atupe taarifa kuwa yeye ndiye aliyemilikishwa hii eka badala ya yule wa awali ambae tumeishi nae kwa amani,” alieleza mmoja ya wananchi hao.