WAPENZI wasomaji wetu leo hii tunaendelea tena na mapishi ambapo kwa makusudi nimewatayarishi pishi la halua.
Kama tunavyojua kuwa pishi la halua ni maarufu sana hapa Zanzibar hasa katika shughuli za harusi na misiba imekuwa ikitumika sana halua, kutegemea na uwezo wake mtu, kwani kwa sasa halua ni gharama kubwa kuinunua.
Hata hivyo, upishi huu unaweza kujaribu siku moja moja kujipikia nyumbani kwako na kujilia.
Kuna aina nyingi za kupika halua kama ya ufuta, lozi, njugu nakadhalika, lakini leo nitawafahamisha namna ya kupika halua ya ufuta.
Basi ungana nami katika kukufahamisha namna ya kupika halua
VIPIMO
Kikombe kimoja cha sukari ya rangi
Vikombe viwili vya sukari nyeupe
Vikombe vitano vya unga wa ngano
Vikombe vitatu vya maji
Kijiko kimoja cha chai kungu manga
Zafarani kijiko kimoja cha chai
Hiliki kijiko kimoja cha chai
Mafuta ya kula vikombe viwili/unaweza tumia samli fresh
Ufuta vijiko vitatu vya chakula
Lozi vijiko 3 vya chakula
Kwa kawaida Halua hupikwa kwa saa moja
NAMNA YA KUPIKA
Chukua bakuli kubwa weka sukari zote nyeupe na rangi, hiliki, kungu manga,weka maji, na unga koroga hadi kila kitu kilainike yaani sukari na unga.
Weka sufiria yako jikoni iwe kubwa kiasi mimina mafuta au samli iache hadi ipate moto sana mimina ule mchanganyiko wako.
Koroga bila ya kupumzika ikifika dakika 45 weka ufuta wako/lozi, halafu koroga hadi itimie saa moja.
Hapo Halua yako itakuwa tayari, Paka sinia mafuta mimina Halua yako iache ipoe tayari kwa kuliwa.