NEW YORK,MAREKANI

POLISI wa jimbo la New York nchini Marekani wanachunguza kituo kimoja cha afya kuhusiana na tuhuma za kujipatia chanjo kwa udanganyifu na kuwapa watu wasio kipaumbele cha kupokea chanjo hiyo.

Mamlaka za afya jimboni humo zilitoa taarifa kuhusiana na shutuma hizo ,zilisema kituo kimoja kinachoendeshwa na mtandao wa afya ya jamii wa ParCare wenye makao yake mjini New York huenda kilijipatia chanjo hiyo kwa kutumia fomu ya maombi isiyo halali.

Aidha mamlaka zilisema chanjo hiyo huenda imekuwa ikipelekwa kwa umma kinyume cha mpango wa jimbo hilo wa kuitoa chanjo kwanza kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele, na pia wakaazi wa makaazi ya kuwatunza wazee na wafanyakazi wake.

Toleo la mtandaoni la gazeti la New York Times lilimnukuu mwakilishi wa kituo hicho akisema kwamba dozi 2,300 za chanjo zilipokelewa kutoka mamlaka za afya za jimbo hilo na dozi 850 tayari zimetolewa kwa mujibu wa miongozo ya mamlaka za jimbo hilo.

Katika mkutano na wanahabari, gavana wa New York Andrew Cuomo alisema mamlaka hazitavumilia udanganyifu wowote katika mchakato wa utoaji chanjo.

Pia alisema yoyote anayejihusisha na udanganyifu atawajibishwa.Alisema atasaini agizo linalosema kwamba ukiukaji wa miongozo ya jimbo hilo utatozwa faini ya hadi dola milioni moja na kwamba matabibu na wauguzi wanaweza kupoteza leseni zao.