NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

MFANYABIASHARA maarufu wa Madini ya Tanzanite Mkoani Arusha, Lucas Mdemu na Polisi wanne wa wanashikiliwa na jeshi la polisi Mkoani Arusha kwa tuhuma za utapeli wa kujipatia fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 15 kutoka kwa mmoja wa mfanyabiashara mkubwa wa madini hayo Mkoani Arusha. 

Kamanda wa Polisi Arusha {RPC},Salumu Hamduni amethibitisha kukamatwa kwa polisi na mfanyabiashara Mdemu na kusema kuwa uchunguzi wa tukio hilo ukikamilika taarifa rasmi zitatolewa kwa vyombo vya Habari. 

‘’Ni kweli tunawashikilia Polisi wanne na mfanyabiashara huyo ila bado tuko katika uchunguzi na uchunguzi ukikamilika tutatoa taarifa rasmi ‘’alisema Kamanda Hamduni

Habari kutoka ndani ya jeshi la polisi Arusha vinadai kuwa polisi hao baadhi yao wakitoka makao makuu ya jeshi  jijini Dodoma ,walipewa dili na mfanyabishara huyo kwenda ofisini kwa mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite ambaye pia ni kiongozi Mkuu wa Chama cha wauzaji madini ndani na nje {TAMIDA} kwa kujitambulisha kuwa  wao ni maofisa kutoka kamati maalumu {Task Force} Makao makuu Jijini Dodoma. 

Kigogo huyo wa TAMIDA {jina linahifadhiwa} alikamatwa na polisi hao waliojitambulisha kutoka kamati maalumu Dodoma na kutaka shilingi milioni 30 ili waweze kumwachia, kwani anatuhumiwa kukwepa Kodi na  hivyo kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.