NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

MTENDAJI Mkuu wa Klabu ya Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Poppat’, ametamba kutumia dirisha dogo la usajili kusajili mshambuliaji wa kimataifa ili kuimarisha kikosi chao.

Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu jana, ‘Poppat’ alisema hatua hiyo inafuatia klabu hiyo kumuuza mchezaji wao Alain Thierry Akono Akono, raia wa Cameroon kwa timu ya Negeri Sembilan ya Malaysia.

Alisema ili kuongeza uimara wa safu hiyo na kuziba pengo la Akono, wana mpango wa kushusha mshambuliaji mwengine kutokana na madhaifu wameyaona kwenye kikosi chao.

“Tumemuuza Akono kwa maslahi mazuri lakini wiki hii tutashusha mshambuliaji mwingine mzuri zaidi,” alisema ‘Poppat’ bila ya kufafanua zaidi.

Kuhusiana na dau la Akono, alisema hawawezi kuweka wazi kiasi gani kimepatikana kwa kuwa hawana utaratibu wa kutaja kiwango au mapato ya wachezaji wanaowauza au kuwasajili hadharani kama ilivyo kwa baadhi ya vilabu vya ndani au nje ya nchi.