MOSCOW,URUSI

RAIS wa Urusi Vladimir Putin amesaini sheria mpya inayompa kinga ya kisiasa milele.

Sheria hiyo inamaanisha kuwa rais huyo na familia yake hawatoweza kufunguliwa mashitaka yoyote hata baada ya kuondoka madarakani.

Awali, viongozi wa Urusi walikuwa na kinga ya kisiasa wakati wakiwa madarakani lakini kuanzia sasa kinga hiyo itamlinda kiongozi kutoshItakiwa kwa makosa yoyote hata baada ya kuachia madaraka.

Njia pekee ya kumvua kinga hiyo ni pale tu kiongozi atakapokuwa anashutumiwa kwa kosa kubwa la uhaini au la uhalifu.

Na hilo nalo litahitaji mchakato mrefu wa kisiasa. Awali mwaka huu, Putin alipitisha marekebisho kadhaa ya katiba ambayo yatamuwezesha kubakia madarakani hadi mwaka 2036.

Hadi hivi sasa bado hakuweka wazi iwapo anadhamiria kugombea tena katika uchaguzi ujao wa mwaka 2024.