NA MARYAM HASSAN

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti akiwemo raia wa kigeni aliyefariki katika hoteli ya Park Hyatt.

Raia huyo wa Urusi ametambulika kwa jina la Sosin Cocnh (53), alikutwa amefariki katika chumba namba 3216 kilichopo ghorofa ya pili ya hoteli hio iliyopo Mji Mkongwe, Zanzibar Disemba 23 mwaka huu, saa 02:00 usiku.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharib Awadh Juma Haji ameeleza kuwa marehemu huyo alifika Zanzibar Disemba 17 mwaka huu kwa shughuli za kitalii pamoja na kutafuta biashara za kuwekeza akiwa na pasi ya kusafiria namba RUS 753612048.

Alisema marehemu huyo kabla ya kifo chake alikuwa amelala na Arafa Ramadhani Mpondo (23) mkaazi wa Fuoni ambae anasadikiwa kuwa ni mpenzi wake aliyempata kwa njia ya mtandao.

 Alisema majira ya saa 5:45 za usiku alimuona marehemu hayuko vizuri na kuamua kulala naye hadi asubuhi na alipomuasha alishindwa kuamka na kuamua kawajuilisha watendaji wa hoteli hiyo kwa ajili ya hatua zaidi.

Alieleza kuwa marehemu alipelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja na majira ya saa 5:51 asubuhi kwa kufanyiwa uchunguzi uliosimamiwa na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 17.

Akizungumza kusuhu mwanamke alielala na marehemu, Kamanda Awadh alisema bado anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano Zaidi huku wakisubiri majibu ya uchunguzi wa kidaktari ingawa hadi sasa imebainika kuwa marehemu alikufa kifo cha kawaida.

Msemaji wa Hospitali ya Mnazimmoja Hassan Mcha Makame, alisema mwili wa marehemu umetolewa damu kwa uchunguzi zaidi wa kimaabara na kwamba mwili wa marehemu umekabidhiwa jamaa zake na umesafirishwa nchini kwao kwa mazishi.

Wakati huo huo Kamanda Awadh alisema siku hiyo hiyo majira ya saa 17:30 jioni huko katika hotel ya Zanzibar Beach Resort iliyopo wilaya ya Magharibi ‘B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja mtoto Nadra Abdulrazak Haji (3), mkaazi wa Beit el Ras wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja akiwa na wazazi wake huko katika hoteli hiyo alifariki dunia mara baada kuzama katika bwawa la kuogelea alipokuwa akiogelea na wenzake.

Alisema marehemu alikimbizwa katika hospitali ya Al-rahma kwa matibabu lakini alikuwa ameshafariki dunia.

Nadra alikuja Zanzibar na wazazi wake ambao waliokuja Tanzania kwa likizo ya mwisho wa mwaka wakitokea Uingereza wanapoishi na kukutwa na umauti.

Hivyo aliwataka wazazi kuwa makini na watoto wao hasa wanapofika katika sehemu za fukwe kwa ajili ya kuogolea ili kuepusha vifo visivyo vya lazima.

“Japo kuwa kifo kinapangwa na Mungu lakini kuna dalili za uzembe wa wazazi wake kwani haiwezekani mtoto wa miaka mitatu akaachiwa akaogelee bila ya uangalizi wa wazazi wake,” alieleza Kamanda Awadh.

Mwili wa marehemu huyo umekabidhiwa jamaa zake kwa mazishi na kwamba kamanda huyo wa polisi aliwataka wazazi kuwa waangalifu na watoto wanapokuwa katika shughuli na michezo inayohitaji uangalizi wa watu wazima.