CAIRO,Misri
RAIS mpya wa Zamalek, Ahmed Bakry, amefariki kutokana na maradhi ya ‘corona’, klabu hiyo imethibitisha.
Bodi ya Zamalek na rais wa zamani, Mortada Mansour, walisimamishwa na Wizara ya Michezo mwezi uliopita baada ya kupatikana kwa ukiukaji wa kifedha na kupelekwa kwenye Mashtaka ya Umma ya Misri huku uchunguzi ukiendelea.


Walibadilishwa na kamati ya muda iliyoongozwa na mjumbe wa zamani wa bodi ya klabu na rais wa Mahakama ya Rufaa huko Cairo, Ahmed Bakry.Bakry alikuwa ameambukizwa ‘corona’ na alitumia wiki kwa kujitenga kabla ya kufariki juzi.

“Kamati inayosimamia Zamalek na wafanyakazi wote wa klabu wanatoa pole zao za dhati kwa familia ya Ahmed Bakry, mkuu wa kamati inayosimamia klabu, aliyefariki asubuhi ya leo (juzi),” Zamalek ilisema katika taarifa.Makamu wa rais wa kamati ya Zamalek inayosimamia klabu, Hisham Ibrahim, sasa atawaongoza ‘Weupe’ hao kwa muda hadi Waziri wa Michezo, Ashraf Sobhi, atakapotangaza rais mpya. (Goal).