NA MWANAJUMA MMANGA

BARAZA la Mji Wilaya ya Kaskazini ‘B’, limetakiwa kulipa fedha za muda wa ziada pamoja na posho la likizo kwa wafanyakazi wake kwa kuzingatia sheria na miongozo ya utumishi wa umma.

Agizo hilo, limetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Rajab Ali Rajab, wakati akizungumza katika kikao cha pamoja na watendaji wa ofisi hiyo huko Kinduni kwa lengo la kusikiliza matatizo ya wafanyakazi na kuyapatia ufumbuzi.

Alisema ili kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa watendaji hao ni vyema kwa uongozi wa baraza la mji kuwa na utaratibu wa kulipa stahiki za wafanyakazi kwa wakati na bila ya upendeleo sambamba na kuwapangia kazi kulingana na taaluma zao.

“Niwaombe sana viongozi ninakitaka kila kitengo kuwa na mpango kazi wake pamoja na kuondoa urasimu kwa wananchi wanaotaka huduma, ili kuwaondoshea usumbufu pale wanapohitaji huduma kwao” alisema Rajab.

Alisema si jambo jema kwa wafanyakazi kutolipwa stahiki zao kwa kisingizo cha madai kuwa fedha hamna ama masuala mengine, hivyo mkuu huyo aliwataka kulipwa wafanyakazi stahiki zao.

Akitoa ufafanuzi kwa baadhi ya matatizo ya wafanyakazi Kaimu Mkurugenzi wa baraza hilo, Patima Omar Ussi, alisema tayari washaorodhesha majina ya wafanyakazi wote wa mkataba  na wale wanaodai stahiki zao, ili kufanya malipo.

Hata hivyo, aliahidi kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya ili kila mfanyakazi aweze kupata stahiki zao.

Mapema wakiwasilisha matatizo yao mbele ya Mkuu wa Wilaya baadhi ya wafanyakazi hao wamesema wamekuwa na ukosefu wa vitendea kazi, uhaba wa ofisi pamoja na usafiri kwa ajili ya kwenda katika maeneo ya kazi.

Hivyo, walimuomba mkuu huyo kuyafanyia kazi yale yote matatizo yanayowakabili ili wafanye kazi kwa uweledi zaidi.