NA HAFSA GOLO
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema hajaridhishwa na kasoro mbali mbali zilizojitokeza katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Kivunge.
Ayoub alieleza hayo wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mkokotoni mkoani humo.
Alisema ujenzi wa hospitali hiyo umetumia fedha nyingi za serikali zipatazo bilioni 4, hadi kukamilika kwake lakini umekuwa na matatizo ambayo yanayochangia kutokuwa na ubora na usalama kwa watumiaji.
“Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Kivunge umekabidhiwa mwezi wa Aprili, mwaka huu, lakini cha kushangaza baadhi ya kuta zimeanza kupasuka na mtiririko wa huduma ya maji haupo kwa kiwango kinachostahiki”,alisema.
Aidha Mkuu wa Mkoa huo kutokana na kutoridhishwa na kasoro zilizojitokeza katika mradi huo ameamua kuunda timu ya watu watano kutoka idara tofauti ikiongozwa na mtendaji wa Wakala wa mjengo ya serikali,Mamlaka ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), usalama wa mkoa, mshauri elekezi, Bado ya mkandarasi na Injinia ili kuchunguza kwa kitaalamu.
Alifahamisha kwamba mbali na uundaji wa timu hiyo pia ataunda timu nyengine mbadala ya siri ambayo nayo pia itafatilia kwa karibu suala hilo na hatimae kuweza kupatikana taarifa sahihi kwa maslahi ya taifa na umma.
“Hatuwezi kuvumilia wala kufumbia macho miradi ya serikali iwe kama shamba la bibi wajanja wachache wanufaike”,alisema.
Mbali na hatua hiyo alisema, iwapo jengo hilo likibainika halipo salama kwa watumiaji atasitisha huduma mara moja hadi pale litakapofanyiwa matengenezo.
Alisema miongoni mwa hatua nyengine atakazochukua mara baada ya kupatiwa taarifa ikiwa ni pamoja na kumtaka mkandarasi kurudisha fedha zote, huku mshauri elekezi kuwajibishwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria.
Sambamba na hilo,alisema hatua nyengine atakayoifanya ni kuwasilisha ripoti kamili serikali kwa hatua zaidi.
Katika hatua nyengine Ayuob alisema,katika ziara zake hajaridhishwa na malalamiko tofauti yaliotolewa na wananchi wa mkoa huo yanayohusiana na vitendo vya dhulma,manyanyaso pamoja na kutolipwa fidia stahiki.
“Hivi ninavyozungumza na mwandishi wewe hapa katika meza yangu yapo malalamiko zaidi ya 100 yaliofikishwa kwa njia ya maandishi”,alisema.
Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi alisema,suala hilo limechukua nafasi kubwa hasa kwa wazawa.
Hata hivyo alisema ,katika kuhakikisha changamoto hiyo inapungua ameandaa mpango kazi ambao utasaidia kutoa fursa na haki sawa kwa wazawa na wawekezaji.
Alifahamisha kwa hatua ya awali ameanza kufanya mazungumzo ya pamoja kati ya muwekezaji wa mradi wa Hoteli na Makaazi na wananchi utakaojengwa Kendwa, ili kuona kila mmoja kwa nafasi yake anaweza kunufaika.