MZEE GEORGE

MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana Mustafa, ameonya vikali tabia ya maofisa ustawi wa jamii na maofisa wanawake na watoto kwa kushindwa kusimamia ipasavyo haki za watoto na wanawake ndani ya Mkoa huo.

Onyo hilo amelitoa kufuatia malalamiko yaliyotolewa na mjumbe wa Shehia ya Dole, Lemi Shija Mbaya, kuhusu mwananchi mmoja anayetuhumiwa kuwadhalilisha watoto wake wawili, kukabidhiwa watoto hao kuwalea badala ya kuwakabidhi kwa mama yao.

Akizungumza katika kikao chake na wafanyakazi wa wilaya na Manispaa Magharibi ‘B’, aliwataka maofisa ustawi wa jamii, wanawake na watoto waliopewa jukumu la kusimamia haki za wanawake na watoto katika mkoa huo kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Alisema bado kuna changamoto kwa jeshi la polisi na watendaji katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji, hivyo hatakuwa na muhali kwa mtumishi yoyote yule atakaeshindwa kutimiza wajibu wake dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

“Nitahakikisha napambana kwa nguvu zangu zote kupinga vitendo vya udhalilishaji na vile vinavyoenda kinyume na maadili ya wazanzibari,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Aliwataka wafanyakazi hao kufahamu kuwa wapo watu wanaofadhiliwa kwa ajili ya kushajiisha vitendo vya udhalilishaji na kuwataka wafanyakazi hao kuongeza bidii katika kupambana na vitendo vya aina hiyo.

Kwa upande mwengine Idrisa aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa kutowalinda ndugu, jamaa au waume zao wanaofanya vitendo hivyo.

“Kuwakinga watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji haitasaidia bali itachangia kushamiri kwa vitendo hivyo,” alisema Idrisa.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ kulifanyia kazi lalamiko hilo na kumpa taarifa na kuahidi kuendelea kulifatilia ili kuona hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

Akielezea kuhusu kadhia hiyo, Lemi alisema hajafurahishwa na uamuzi uliotolewa wa kukabidhiwa watoto wanaodaiwa kuingiliwa na baba huyo kwake jambo ambalo limethibitishwa na madaktari waliowachunguza watoto hao.

Alisema kitendo cha kumpa baba huyo watoto hao baada ya kuachiwa kwa dhamana, sio sahihi kwani kinawezq kumpa nafasi baba huyo kuendelea kuwafanyia watoto hao uovu huo.

Hivyo alisema shauri hilo ni la muda mrefu na kwamba linaonekana kutoshughulikiwa kikamilifu hivyo alimuomba mkuu huyo wa mkoa kufuatilia uendeshaji wa kesi hiyo ili haki itendeke.