NA JOSEPH NGILISHO ARUSHA

MKUU  wa Mkoa wa Arusha,  Iddy  Kimanta,  amelaani vikali   udanganyifu uliofanywa na shule tatu  binafsi za msingi mkoani humo  katika mtihani wa darasa la saba na kupelekea matokeo ya wanafunzi  hao kufutwa.

Kimanta alilaani kitendo hicho jana  wakati akifungua kikao cha uchaguzi wa wanafunzi waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya nsingi na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2021. 

Alisema kuwa  kitendo hicho kimeharibu sifa ya Arusha na kufanya miaka saba ya watoto ambao matokeo yao yamefutwa kuwa bure, jambo ambalo halikubaliki baada ya shule za mchepuo wa kingereza ikiwemo  Precious ya halmashauri ya Meru, Eunoto ya wilaya ya Monduli pamoja na Dominion ya Arusha Jiji.

“Jambo hili halikubaliki limepelekea watoto kupata adhabu ya kufutiwa matokeo kwa kuponzwa na watu wazima ambao wanahitaji sifa wasizostahili,”Alisema Kimanta.

Alieleza kuwa ili wapate sifa wafundishe  kama ambavyo taratibu na kanuni zinaelekeza na sio kufanya vitendo viovu vinavyoleta aibu na kuharibu sifa ya mkoa.

Alifafanua kuwa mkoa wa Arusha una mikakati  ya kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda, hivyo alitoa rai kwa shule binafsi kuhakikisha wanafuata taratibu na sheria na kutafakari wanachotakiwa kufanya  kwa maslahi ya taifa.

Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha Emmanuel Maundo alisema mwaka 2014 jumla ya wanafunzi  44,754 wavulana wakiwa  22, 357 na wasichana  22,447 walianza darasa la kwanza na waliosajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba walikuwa elfu 40,729 wavulana wakiwa ni  20,059 na wasichana  20,670.

Alieleza kuwa waliofanya mtihani ni wanafunzi  40,192 wavulana wakiwa ni  19,730 na wasichana 20,462 ambapo waliofaulu ni wanafunzi elfu 37,057 wavulana wakiwa ni  17,864 na wasichana 19,193 ambapo ni sawa na asilimia 92.42.

“ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.75 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2019 ambao ulikuwa ni asilimia 91.67 ambapo kwa sasa ongezeko la wanafunzi waliofaulu ni elfu 2,548 na kupelekea Arusha kushika nafasi ya pili kitaifa,” Alisema.

Naye katibu tawala wa mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, alisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa awamu ya kwanza ni wanafunzi  34,263 wasichana wakiwa ni  17,762 na wavulana wakiwa ni  16,501 sawa na asilimia 94.4 .