NA TATU MAKAME

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema iwapo miradi ya serikali itatekelezwa kwa kushirikiana na  wakala wa majengo, matatizo mengi yanaweza kupungua.

Alisema hayo ofisini kwake Mkokotoni wilaya ya kaskazini ‘A’ alipokuwa akipokea ripoti ya kamati ya wataalamu inayochunguza nyufa katika jengo la mama na mtoto la hospitali ya Kivunge.

Alisema serikali ya mkoa haitawakumbatia wakandarasi wababaishaji, hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa kama nyufa hizo zimesababishwa na uzembe.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mkurugenzi wa wakala wa majengo Zanzibar, Ramadhan Mussa Bakari, akikabidhi ripoti hiyo alisema kamati itakutana na mkandarasi,wizara ya afya na wakala wa majengo.

Nao wananchi wa mkoa huo walimuomba Mkuu wa Mkoa kuwafuatilia wakandarasi waliojenga wodi hiyo na kuchukulia hatua.

Kamati hiyo iliundwa baada ya Ayoub kutembelea hospitali hiyo na kubaini kasoro nyingi.