NA ASYA HASSAN
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amewasisitiza madaktari na wauguzi wa vituo vya afya kufuata sheria na taratibu za kiutendaji wa kazi zao kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema lengo la serikali ni kuimarisha huduma za afya hasa za mama na mtoto, ni kuona wananchi wanapata huduma zinazostahiki bila ya usumbufu.
Mkuu huyo, alifahamisha kwamba si jambo la busara kuona baadhi ya wahudumu wanakwenda kinyume na sheria na maadili ya kiutendaji hali ambayo inapelekea kuleta malalamiko na kuitia doa serikali.
Aliyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika vituo vya Uzini, Bambi na Umbuji, ili kuona utolewaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili watendaji wa vituo hivyo.
Akizungumzia kuhusu suala la wafanyakazi kufunga kituo cha afya Bambi, alisema serikali haikuridhishwa na suala hilo na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wa suala hilo.
Kwa upande wa baadhi ya wahudumu na madaktari wa vituo hivyo walisema wanakabiliwa na uhaba wa wafanya kazi pamoja na posho la likizo na kutopata huduma ya maji hasa katika vituo vinavyotoa huduma za mama na mtoto.
Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kati, Mohammed Salum Mohammed, aliwashauri wakuu wa vituo kuwa changamoto zinazojitokeza katika utendaji wao isiwe ni kigezo kukwamisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.