NA MWANDISHI WETU, RUKWA

SERIKALI Mkoani Rukwa kwa kushirikiana na Kiwanda cha Alpha Tanganyika Flavour Ltd, imezindua siku ya Uhamasishaji wa kula Samaki mkoani humo.

Uamuzi huo umefanyika kwa lengo la kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya mchanganyiko wa vyakula vya makundi tofauti yanayozalishwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huku msisitizo ukitolewa katika ulaji wa samaki.

Tafiti zinaonesha kuwa hali ya udumavu na utapiamlo kwa Watoto walio na umri chini ya miaka mitano mkoani humo imeshuka kutoka asilimia 56.3 ya mwaka 2016 hadi asilimia 47.9.

Hiyo ikiwa ni kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na mkoa katika kupambana na matatizo ambayo yanasababishwa na ulaji wa chakula cha aina moja hasa kundi la chakula cha wanga, kuliko makundi mengine ya vyakula hasa protini.

Akizungumza kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakati wa uzinduzi wa siku hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Khalfan Haule, amesema kuwa Mkoa huo una vyanzo vingi vya uzalishaji wa samaki ikiwemo Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa, Bwawa la Sundu, Bwawa la Kwela Pamoja na mabwawa 328 yaliyopo katika maeneo mbalimbali ya mkoa.

Aidha, Alisema kuwa kwa mwaka 2018/2019 na 2019/2020 wastani wat ani 2,444.323 za samaki zimevuliwa katika vyanzo hivyo vya uvuvi, na kuongeza kuwa asilimia 15 hadi 30 ya mwili wa samaki ni protini na mafuta ya samaki yana Omega 3.

Alisema hali hiyo, imeonyesha kuwa ni mafuta bora na salama katika mwili wa binadamu, kwani hayasababishi maradhi ya moyo kama yalivyo mengine.

“Ndugu Washiriki sisi kama serikali tutaendelea kushirikiana na mwekezaji Alpha Tanganyika Flavor Ltd katika kuhakikisha kuwa tunawahamasisha wananchi wa mkoa wa Rukwa kula Samaki ili wawe na soko namba moja la kiwanda cha Alpha Tanganyika kwenye mkoa wetu wa Rukwa, nikuhimize mchakate samaki kwa ubora wa kiwango kinachohitajika katika soko la ndani na nje ya mkoa n ahata nje ya nchi ili uutangaze mkoa wetu kupitia zao hili la samaki,” Alisema.