NA HALIMA JUMA

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba,  Mattar Zahor Nassor, amewataka vijana kutumia nafasi zao katika kuwaunganisha wananchi na serikali yao.

Aliyasema hayo ofisini kwake wakati akizungumza na viongozi na wajumbe wa taasisi ya Mimi na Mwinyi Zanzibar, ambao walifanya ziara zao kisiwani hapa.


Alisema vijana ndio nguvu kazi ya taifa katika kuleta maendeleo, hivyo ni busara kutumia fursa hizo kuwa madaraja ya  kuwaunganisha vijana wengine, ili kutoa mwamko ambao  utawajenga kuwa wazalendo wa nchi yao.


Aidha aliwataka kuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii, kuhusu dhamira alionayo Dk. Mwinyi katika kuleta mageuzi ya utendaji bora kwa maendeleo ya wananchi.

Mapema Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Salmin Shukuru Botea, alisema lengo la ziara hio ni pamoja na kukutana na makundi mbalimbali katika kuhamasisha jamii kuitambua serikali yao.


Nae Msimamizi ya taasisi hio kisiwani Pemba, Mohammed Said Soud, alisema taasisi hiyo imeandaa mikakati maalum ya kuutangaza uchumi wa buluu, ikiwemo suala la utalii wa ndani kwa kutembelea sehemu za kihistoria zilizomo kisiwani Pemba.

Taasisi ya Mimi na Mwinyi ni miongoni mwa kundi lililoshiriki kikamilifu katika kampeni za mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambae kwa sasa ni Rais wa Zanzibar.