NA ABDI SULEIMAN

MSAIDIZI Mkurugenzi wa huduma za kijamii na afya ya Msingi kutoka Baraza la Maji Chake Chake Dk.Moh’d Ali Jape, amesema anasikitishwa na baadhi ya wazee kurudisha nyuma juhudi za serikali pamoja na mashirika mbali mbali yanayojitokeza kusadia huduma za afya kwa watoto.

Alisema kumekua na baadhi ya wazee wanashindwa kuwapeleka watoto wao hospitali kupatiwa huduma ya afya, kwa kisingizo cha kutokua na nauli au kujali kwenda shamba kulima, wakati mashirika hayo yameshatoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwahudumia watoto hao.

Hayo aliyaeleza huko skuli ya sekondari Vitongo Wilaya ya Chake Chake, wakati alipokua akikabidhi kadi 44 za Bima ya afya kwa wazazi na walezi wanaolea watoto ambao wamo katika mradi wakuimarisha familia unaotekelezwa na shirika la SOS Pemba.

Aidha aliwataka wazee kuthamini juhudi zinazotolewa na taasisi binafsi, ikiwemo shirika la SOS kwa kuwafikisha watoto wao spitali kupatiwa matibabu pale wanapoumwa.

“SOS ni moja ya mashirika yaliyokua mstari wa mbele kusaidia huduma za jamii, leo wapo kwa ajili ya kuwapatia Bima ya afya hili ni jambo kubwa kwenu wazazi”alisema.

Hata hivyo, Dk.Jape, alilipongeza shirika la SOS, kuwa mastari wambele katika mapambano ya kuleta maendeleo, kwa kuhakikisha watoto wanapata afya bora kwani bila ya afya hakuna kitu kitakachofanikiwa.

Kwa upande wake Mratib wa Miradi kutoka shirika la SOS Pemba, Ghalib Abdalla Hamad aliwataka wazazi na walezi kuzitumia ipasavyo kadi za bima ya afya walizopatiwa kwa lengo na kutatua changamoto za afya katika matibabu yanayowasumbua.

Alisema lengo la SOS ni kuwajengea mustakbali bora watoto katika suala zima la Afya, kwa kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, afya bora ili kuona wanaishi katika mazingira mazuri.

“Hizi bima za afya wengi wamekuwa wakizizarau, lakini zimekuwa na mchango kubwa kwa nchi katika kutatua changamoto ya afya kwa wanananchi, wakatia wanapopatwa na tatizo”alisema.

Naye Makame Haji kutoka SOS Pemba, alisema suala la afya ni kitu muhimu kadi hizo ni muhimu sana hivyo haiwezekani kuziwacha majumbani.

Kwa upande wao walezi na wazazi waliokabidhia kadi hizo kwa niaba ya watoto wao, walilishukuru shirika la SOS kwa kuwapatia bima hizo za afya, kwani zitaweza kuwasaidia kwa kuwapeleka watoto wao spitali pale watakapoumwa.

Shirika la SOS Pemba limekusudia kukabidhi kadi 71 kwa watoto wa shehia tatu, Vitongozi watoto 44, Chonga watoto 24 na michenzani watoto watatu, kadi hizo ziliwa zimegharimu shilingi Milioni 3,578400/= zikianza kutumika kuanzia 2020 hadi 2023.