NA ASIA MWALIM

KIJIJI Cha S.O.S kimezindua mradi wa maji safi na mazingira ambao utagharimu  thamani ya Europe128,172 sawa na T Shilingi  3,606,1500 kwa wanakijiji wa shehia za Tumbatu ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa maji nchini .

Afisa Mradi wa Kuimarisha Familia Kijiji  cha S.O.S Zanzibar ,Zakaria Khamis Shame, alizindua mradi huo huko Tumbatu Kichangani Kaskazini Zanzibar.

Afisa huyo, alisema Tumbatu ni kijiji  moja wapo kinacho kabiliwa na upungufu wa  upatikanaji maji kutokana na kutanuka  kwa kijiji hicho sambamba na ongezeko la idadi kubwa ya watu.

Alieleza kuwa miundo mbinu ya maji safi na salama ni muhimu katika harakati za kila siku kwa maisha ya binaadamu hivyo mradi huo utasaidia kutatua changamoto hiyo kwa wananchi wa kijiji hicho.

Alifahamisha kuwa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya maji Zanzibar(ZAWA) imechukua juhudi kubwa katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa maji, kwa kupeleka bomba la kusambazia maji kwa awamu tofauti .

Alieleza kuwa mwaka 1978 ZAWA ilifanikiwa  kupeleka mfumo wa bomba la saruji (AC system)lenye upana wa inchi nne na urefu wa mita11, 673, ambapo lilianzia mkokotoni hadi Tumbatu na kufika baadhi ya maeneo.

Aidha mnamo mwaka 2005 – 2011 ilifanikiwa kupeleka mfumo mwengine wa  ‘HDPE system’, ambao ina urefu wa mita 24,090  system ambao ilitokea kisima cha Kipange hadi Tumbatu, baada ya kugundua kuwa mfumo wa awali ni mdogo na  haukidhi mahitaji ya wanakijiji hicho.

“Utafiti wa serekali na wafadhili umegundua kuwa kuunganishwa bomba zenye nchi nne, tano na tisa hadi11 ndio chanzo cha tatizo la maji kutokana na ukubwa tofauti wa bomba” alisema.

Alifahamisha kuwa lengo la mradi huo ni kuondoa  changamoto ya maji kijijini hapo,  kwa kununua mabomba na matenki, yatakayo sambaza maji sehemu muhimu ikiwemo vituo vya afya, skuli na majumbani.

Alieleza lengo jengine ni ukarabati wa vyoo vya skuli, kibanda cha kuhifadhia mashine ya maji kipanga sambamba na kutoa mafunzo ya ufundi na utaalamu wa mashine za maji kwa baadhi ya vijana.

Aidha alisema mbali na mradi huo kutoa huduma ya maji kwa wananchi hao pia wanatakiwa kudumisha usafi wa mazingira ndani ya skuli, vituo vya afya,na kijiji kiujumla ikiwa ni sehemu ya mradi huo.

Nae Diwani wa wadi hiyo, Makame Ali Chumu, aliishukukuru Serekali kwa kuwapatia wafadhili watakao saidia kuleta maji yatakayo tosheleza na yenye uhakika kijiji hapo.

Aidha aliomba wafadhili hao kuwapatia matenki makubwa yenye uwezo wa kutoa maji kila siku bila ya mgao, ili kuondokana na changamoto hiyo iliyowakumba kwa muda mrefu .

Nao wananchi wa kijiji hicho wamesema mradi huo utaweza kubadilisha mfumo wa upatikanaji huduma ya maji kijijini hapo, sambamba na kuongeza hatua ya kutaka  wataalamu waweze kutoka kijijini hapo kwani ndio wanaojua matatizo yao.

“Tukiwa na wataalamu wetu hapa watajua matizo ya kijiji chao hatutosubiri mafundi wa mbali ambao watachukua muda  kutengeneza mashine zinapoharibika” walieleza.

Mradi huo wa mwaka mmoja utahusisha shehia za Tumbatu Kichangani na Jongoe, ambao unatarajiwa kuanza 2021 chini ya wafadhili wa Rambor Foundation kutoka Denmark.