KWA bahati nzuri sana nchi yetu ina sheria nyingi na nyengine zimekuwa zikitungwa au kurekebishwa kila pale inapoonekana kuna haja na umuhimu wa kufanywa marekebisho ama kutungwa mpya.

Kuwepo sheria na kuzitii ni vitu viwili tofauti, kwani ukweli ni kwamba miongoni mwetu wapo watu wanaojiona hawahusiki utii wa sheria kama kwamba sheria hizo zimetungwa kwa baadhi ya watu.

Watu kama hawa ambao wengi wanaringia vyeo, nafasi zao au za watu wanaohusiana nao kifamilia au kirafiki, ni hatari kwa ustawi wa jamii inayotaka kujenga taifa ambalo hakuna yeyote anayenyimwa haki za msingi.

Hawa ndio wale wanaojiona ni ‘Mungu watu’ na kwamba hawastahili kuguswa na sheria, kwa maneno mengine, ni watu wasioweza kuhojiwa au kuulizwa ‘The untouchables’ hata pale wanapofanya mambo yanayokinzana na sheria.

Nchi kama Zanzibar inayotaka kupiga hatua za kimaendeleo kwa haraka haiwezi kufikia huko endapo sheria zitakuwa zinawagusa baadhi ya watu wengine haziwagusi au wengine wanashurutishwa kuzifuata wengine wapewa fursa ya kuzivunja.

Kwa mfano Zanzibar kwa muda mrefu mtu wa kawaida, mtu wa kawaida kwa maana asiye na uluwa ama ushawishi, anaponunua gari na kuiingiza nchini kutoka nje, mamlaka za kodi humkalia kooni lazima alipe kodi, hili ni jambo jema sana.

Mtu huyo husomewa vifungu vya sheria vya kulipa kodi na kwasababu yeye ni mtu wa kawaida hivyo huchukua kila jitihada na kuhakikisha analipa kodi husika na kufanikisha kutolewa kwa gari ama biadhaa zake.

Hata hivyo, hili limekuwa kinyume kabisa na wenye uluwa, wanapoingiza gari au biadhaa mbio hukimbilia wizara ya fedha kuonana na waziri kwenda kuomba msamaha wa kodi ‘exemption’.

Mtu huyo anayekwenda kuomba msamaha wa kodi ana uwezo mkubwa wa kulipa kodi stahiki ya serikali, lakini kwa sababu ya uluwa na kutumia vibaya fursa hukwepa makusudi kulipa kodi.

Wakati mwengine gari iliyoingizwa na mtu mwenye uluwa sio kwa ajili ya matumizi binafsi, bali kwa matumizi ya kibiashara hapa ndipo msemo wa kiswahili unaosema ‘penye fungu ndipo paengezwapo’ unaposibu.