NA HAFSA GOLO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya matibabu kwa waliojeruhiwa kufuatia hapo juzi kuporomoka kwa jumba la Beit- al- Ajaib lililopo Forodhani.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed alieleza hayo jana alipokua akitoa muendelezo wa taarifa kuhusu kuporomoka kwa jumba hilo la kihistoria.

Alisema hatua hiyo ya serikali inaenda sambamba na ushiriki wa kikamilifu katika mazishi ya watu wawili waliopoteza maisha kufuatia tukio hilo ambapo mmoja wa marehemu hao ni Pande Makame Haji mwenye umri wa miaka 25 mkaazi wa Bububu na Burhani Ali Makuno mwenye umri wa miaka 35.

Waziri huyo alisema serikali inaungana na ndugu na jamaa pamoja na wananchi wote wa Zanzibar katika kupokea msiba huo mzito huku akiwataka wafiwa wawe na subira katika kipindi hichi kigumu.

Aidha Waziri huyo alisema, serikali inaendelea kusimamia kwa karibu shughuli zote za operesheni zinazoendelea kuhusiana na tukio hilo ikiwemo utafutaji na uokozi katika eneo la tukio na uondoshaji wa kifusi.

Hata hivyo alichukua fursa hiyo kuvishukuru kwa dhati vikosi vya ulinzi na usalama, wakala wa barabara, mamlaka ya bandari na wahusika wengine wote na wananchi kwa ujumla kwa juhudi zao katika kufanikisha shughuli za utafutaji na uokozi kwani mashirikiano hayo yamesaidia kufanikisha kwa haraka shughuli za uokozi.

Alisema wananchi waendelee kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu na Serikali itaendelea kuwapa taarifa kadri shughuli za operesheni zitakavyokuwa zikiendelea hadi kukamilika kwake.

Mapema waziri huyo alisema katika tukio hilo hadi juzi jumla ya watu wanne waliokolewa wakiwa hai na kufikishwa hospitali ya Mnazimmoja kwa ajili ya matibabu.

Alisema miongoni mwa majeruhi hao ambao bado wanaendelea kupatiwa matibabu ni pamoja na Ali Ramadhan mwenye umri wa miaka 28 mkaazi wa Kinuni na Haji Juma Machano (24) mkaazi wa Chumbuni, Hamad Mattar (35)mkaazi wa Kinuni na Zamir Salum (40) ambae pia ni mkaazi wa Kinuni.