NA NASRA MANZI
KAMPUNI ya Utengenezaji na Uuzaji wa Vifaa vya Michezo (Salient Group, SG Sport), imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu nne za Zanzibar zitakazoshiriki mashindano ya kuwania Kombe la Mapinduzi.


Timu zilizokabidhiwa vifaa ni Jamhuri SC, Mlandege FC,Malindi SC pamoja na Chipukizi United, ambapo makabidhiano hayo yalifanyika katika ukumbi wa judo huko Amani.


Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Masoko wa Kampuni hiyo Nervily Yahya Mchatta, alisema lengo la kuja Zanzibar ni kujitangaza kimasoko pamoja na kuuza ubora wa vifaa vyao vya michezo.


Alisema wameanzia kutoa vifaa hivyo katika mpira wa miguu lakini wataendelea na mikakati ya kuwapatia vifaa na madaraja mengine ili kuibua vipaji kwa vijana.


“Kwa sasa tumejikita na kutoa vifaa katika mashindano ya Mapinduzi lakini kwa baadae tutaandaa mikakati ya kuwapatia madaraja mengine tunafahamu changamoto za vifaa baadhi ya maeneo” alisema
Nazo timu zilizopewa vifaa hivyo zimeelezea kupata faraja kwa kukabidhiwa vifaa hivyo, kwani vitasaidia kuendeleza mpira visiwani na kupatikana vipaji vitakavyosaidia Taifa.


Vifaa vilivyokabidhiwa ikiwemo Jezi, Gloves, Bibs pamoja na mipira.