SHUKRANI zote anastahiki kuabudiwa yeye Allah (SW) na Mtume Muhammad ni mjumbe wake.
Katika makala haya tutazungumzia namna ya athari za sheria za kiislamu katika utekelezaji wake na namna ya kuirekebisha jamii.
Ili kuona kila kitu kinakwenda sawa katika mukhtadha wa kiislamu marekebisho ni jambo linalohitaji subira na juhudi kubwa mno, kwa kuwa kila mmoja ana sifa zake mwenyewe, na kwa mujibu wa kutofautiana kwa sifa na maumbile ya watu ni vigumu kuainisha mfumo mmoja kwa kurekebisha mambo yao.
Kwa hiyo, Mtume (S.A.W.) alikuwa anatumia mbinu na namna mbalimnbali kwa ajili ya kuwaita watu wajiunge na dini na kujiendeleza na kuzirekebisha nafsi zao kutoka ujahili kwa Uislamu na kutoka dhuluma kwa uadilifu.
Sheria ya kiislamu ilizingatia tabia ya kutoa maagizo na makatazo kwa mbinu ya kidogo kidogo kwa mujibu wa maumbile ya watu na hali yao, dalili kubwa zaidi kwa kuthibitisha hayo ni kwamba Qurani Takatifu iliteremshwa kwa mfumo huo huo, maana Qurani ilianza kwa kugusia masuala makuu makuu tena kwa mfumo wa kuwaita watu na kuwafahamisha dini hiyo kidogo kidogo.
Hadithi iliyosimuliwa kutoka kwa Bi Asha (R.A.): “Hakika ya kwanza kuteremshwa kutoka katika Qurani Takatifu ni sura za Mufassal ambazo zinazungumzia moto na pepo kwa kuwa hilo ndilo lango la kwanza la kuwavutia watu kujiunga na dini mpaka wakishajiunga na dini zikaja sura za kubainisha yanayo halali na yanayo haramu yaani maagizo na makatazo, na kama sura za kukataza pombe zikiteremka kwanza wangalikataa kuacha pombe milele”
Kwa hiyo, daawa nzima ilikuwa inafuata mfumo huo wa kutoa maagizo, makatazo, maelezo na hata mafunzo kwa watu kulingana na mbinu hiyo hiyo ya kidogo kidogo, na hata katika jambo moja tunakuta sheria ya kiislamu imefuata mbinu hiyo kama ilivyokuwa wakati wa kukataza pombe.
Kwa kweli pombe ilikatazwa na kuharamishwa kidogo kidogo kwa sababu sheria ya kiislamu ilitambua kiasi watu wa enzi hiyo walivyokuwa wanaipenda sana na kuwa na hamu ya kuikunywa wakati wote.
Pia, baadhi ya ibada na faradhi katika Uislamu zilifaradhishwa kwa mujibu wa mfumo huo huo, kama vile Swala, Saumu na Jihad kwa ajili ya kuziandaa nafsi za waislamu wakubali maagizo haya.
Mbali na hayo, kutimiza jambo kwa mbinu ya kidogo kidogo ni miongoni mwa maumbile yaliyopitishwa na Mwenyezi Mungu (S.W.) kuanzia kuumba kwa ulimwengu wetu huu kwa ardhi na mbingu katika siku sita japo kuwa Mwenyezi Mungu ana uwezo wa kuziumba mara moja tu lakini lada kwa hekima ya kutufundisha kwamba mbinu hiyo ni sehemu ya maumbile aliyoyaweka Mwenyezi Mungu.
{Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, MolaMlezi wa viumbe vyote} [7/54].
Jambo jingine linalobainisha ukweli huu ni kuumba kwa mwanadamu mwenyewe, ambapo mfumo wa kidogo kidogo ndio mfumo unaoelezwa katika kumwumba mwanadamu kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.): {Na kwa yakini tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo * Kisha tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti * Kisha tukaiumba tone kuwa damu iliyo ganda, na tukaiumba damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji} [23/ 12-14].
Ujumbe wenyewe wa Mtume (S.A.W.) ulichukua muda wa miaka 13 kwa kuzingatia hali ya watu wa enzi hiyo ambao walikuwa wameshazoea maisha ya ukafiri, ujinga na maovu kwa hiyo Mtume (S.A.W.) alikuwa anafuata mbinu ya kuwaita watu kwa dini kidogo kidogo na kwa taratibu inayosaidia kufanikiwa katika kazi ya ulinganiaji, enzi ya kwanza ilikuwa ya kutoa wito kisiri siri kisha kutangza dini kisha hijra kisha kuanzisha dola kisha kuweka misingi thabiti ya nchi kisha mambo ya miamala na ibada.
Kutokana na mambo haya tunahakikisha kuwa kazi yoyote inayofanywa kwa utaratibu hufanikiwa na kwamba mfumo wa elimu inayotolewa kidogo kidogo hufika mara moja na kupokelewa vizuri.
Imeandaliwa na Sheikh; Kamal Abdul-Moty Abdul-Wahed
Mkurugenzi wa Kituo cha Kiislamu cha Misri
Dar es Salaam, Tanzania