NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba jana imeibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Ihefu, ikiwani mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara,mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck inafikisha pointi 35 baada ya kucheza mechi 15, ingawa inabaki nafasi ya pili mbele ya vinara, Yanga SC wenye pointi 43 za mechi 17.

Katika mchezo huo  uliochezeshwa na mwamuzi  Nassor Mwinchui wa Pwani aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Geoffrey Msakila wa Geita hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 3-0.

 Simba ilifunguwa akaunti ya mabao kupitia Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dakika ya tisa akimalizia kazi nzuri ya beki wa kulia, Shomari Kapombe.

Mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu misimu miwili mfululizo iliyopita akaifungia Simba SC mabao mawili dakika ya 15 akimalizia pasi ya winga Luis Miqussion kutoka Msumbiji na dakika ya 40 akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chotta Chama.

Mshambuliaji mpya, Chris Mutshimba Kope Mugalu, raia wa Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo (DRC) akakamilisha shagwe za mabao dakika ya 84 akimalizia pasi ya Chama.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Ibrahim Ame/David Kameta dakika 72, Kennedy Juma, Rally Bwalaya, Said Ndemla, Meddie Kagere/Chriss Mugalu dakika 66, Clatous Chama na Luis Miquissone/Hassan Dilunga dakika 75.

Ihefu SC; Deo Munishi ‘Dida’, Mando Mkubwa, Omary Kindamba, Wema Sadoki, Michael Masinda, Samuel Jackson, Juma Mahadhi/Issa Ngoah dakika 47, Willy Mgaya, Andrew Simchimba/ Teps Evance dakika 90, Omary Hamisi/Joseph Kinyozi dakika 47 na Joseph Mahundi.