IWAPO rais Yoweri Museveni atashinda kama inavyotarajiwa katika kinyang’aniro cha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Januari 14 mwakani, akimaliza muhula wake wa ushindi huo atakuwa amekaa madarakani kwa miaka 40.

Museveni atakuwa amekaa madarakani kwa muda mefu kuliko rais mwingine yeyote katika taifa hilo na katika eneo zima la Afrika Mashariki.

Katika nyakati ambazo nchi nyingi za Afrika zimeanza kufuata utaratibu wa kuweka ukomo wa kukaa madarakani, ni vigumu kumuona kiongozi mwingine wa Uganda au nchi nyingine za Afrika Mashariki akikaa madarakani kama au zaidi yake.

Museveni amefanya hivyo katika taifa ambalo kabla yake hakukuwahi kuwa na kiongozi aliyekaa madarakani kwa hata miezi 10, ambapo baadhi ya watangulizi wake Profesa Yusuf Yule na Godfrey Binaisa, wakiwa wamekaa madarakani kwa miezi kadhaa tu.

Suali linaloulizwa na wengi ni kwamba kiongozi huyu vipi amefanikiwa kubaki madarakani kwa muda wote huo? Rais wa kwanza wa Uganda, Milton Obote, aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo mwaka 1972.

Mapinduzi hayo yalifanywa na Jenerali Idi Amin aliyekuja kuitawala Uganda hadi mwaka 1979 alipoondoshwa madarakani na majeshi ya Tanzania yakishirikiana na vikundi vingine vya kijeshi vya Uganda.

Museveni naye aliingia madarakani kupitia vita ya msituni iliyoiondoa madarakani serikali ya Tito Okello Lutwa.

Okello naye aliingia madarakani kwa kumpindua Obote, tena akishirikiana na askari wengine waliokuwa chini ya Museveni.

Kwa hiyo, tangu Uganda ipate Uhuru wake mwaka 1962, nchi hiyo haijawahi kuwa na marais waliobadilishana madarakani kupitia sanduku la kura.

Mara zote, marais hutoka na kuingia kupitia mtutu wa bunduki. Kwa sababu hiyo, ilikuwa lazima kwamba Rais ambaye angedumu madarakani kwanza alitakiwa kuwa na udhibiti wa jeshi.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) la sasa ni mtoto wa Jeshi la Msituni la National Resistance Army (NRA) lililompindua Okello. Hili ni jeshi ambalo Museveni alilisuka mwenyewe akiwa msituni na hadi sasa wale waliokuwa naye msituni wana sauti kubwa ingawa anaingiza damu mpya kila uchao.

Watu kama akina Jenerali Elly Tumwine, Jenerali Caleb Akandwanaho (Salim Saleh) – ambaye ni mdogo wake wa damu, Jenerali David Tinyefuza Sejusa, Kahinda Otafiire na wengine ni watu ambao wako naye kwa takribani miaka 40 sasa.

Kitendo cha kuwa na jeshi linaloundwa na watu wa makabila yote ya Uganda; kinyume cha zamani ambapo asilimia kubwa ya wanajeshi walikuwa wanatoka kaskazini mwa taifa hilo na kulifanya kuwa la kisasa, limempa muda zaidi wa kukaa madarakani.

Rais huyo ni mjanja pia katika kuhakikisha askari wake wa ngazi za juu wanapata maslahi mazuri na pengine ni faida zaidi kwao kuwa naye madarakani kuliko kuwa na mtu mwingine ambaye anaweza kuwabadilikia.

Museveni na jeshi lake la UPDF wamekuwa kama mbuzi na majani; mbuzi akitegemea kushiba kwa kula majani huku majani yakitegemea mbolea kutoka kwa mbuzi ili yakue na kunawiri. Ni uhusiano ambao umemfanya Museveni asalie madarakani bila ya kupinduliwa.

Museveni huyu wa sasa ni tofauti na yule wa miaka yake 10 ya kwanza madarakani baina ya mwaka 1986 hadi mwaka 1996. Wakati alipoingia madarakani, alizungumza na kutenda mambo mazuri yaliyomtofautisha na watangulizi wake wote waliokuwa marais kabla yake.

Alizungumza kuhusu umuhimu wa taifa kuwa na itikadi, tatizo la viongozi wa Afrika kung’ang’ania madarakani hata wanapokuwa wamechokwa na wananchi na aliandika maandishi mazuri ya kimapinduzi yaliyowasisimua watu wake.

Alipoingia madarakani aliikuta nchi ikiwa hoi kiuchumi, wastani wa kipato cha mwananchi wa kawaida ukiwa chini ya dola 35 kwa mtu mmoja, lakini sasa kipato hicho kimeongezeka kwa zaidi ya mara 10.

Alikuta wananchi wa Uganda hasa eneo la kaskazini wakiwa na tishio la kigaidi la kundi la Alice Lakwena lililokuwa likifanya mambo ya maovu kwa wananchi wa Kaskazini ya Uganda na baadaye kundi la kigaidi la Lord Resistance Amy (LRA) lililokuwa likiongozwa na Joseph Kony.

Museveni alipambana na makundi yote mawili na kuyashinda na kuleta amani ya kudumu nchini Uganda.

Uganda pia ilikuwa imeathiriwa sana na ugonjwa wa UKIMWI wakati Museveni anaingia madarakani mwaka 1986 na ni juhudi zake za kisasa katika kukusanya mapato na misaada ndiko kulikopunguza vifo na mateso waliyokuwa wanayapata Waganda wakati huo.

Uganda ya sasa ni yenye amani, uchumi unaokua, heshima katika jamii ya kimataifa na watu wenye afya njema kiasi kwamba taifa hilo ni moja wapo ya yenye watu wanaozaa sana duniani.

Yote hayo ni matunda ya utawala wa Museveni. Kuna wanaomkumbuka na kumuenzi kwa sababu ya mazuri yake hayo aliyoyafanya kwa Uganda.

Tatizo lake ni kwamba sasa wastani wa umri wa mwananchi wa Uganda ni miaka 16, ikimaanisha wengi wa Waganda walio hai hawakushuhudia madhara na matatizo nchi hiyo ilipitia kabla ya Museveni.

Watu hao wamefunua macho na kuiona Uganda ya sasa na wanatamani kuona sura nyingine ikiwa inaongoza taifa hilo.

Katika chaguzi zote zilizofanyika Uganda tangu mwaka 1996, Museveni amekuwa akitumia nafasi yake kama rais na amiri jeshi mkuu wa taifa hilo kuwadhibiti wapinzani wake.

Mara zote, yeye ndiye anayeoneshwa zaidi na televisheni ya serikali ya UBC wakati wa kampeni, anatumia gari na rasilimali nyingine za serikali wakati wa kampeni na anatumia polisi, jeshi na askari wengine wa vikosi visivyo rasmi kuwatisha na kuwapiga washindani wake.

Matokeo yake ni kwamba Uganda haijawahi kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki kwa vyama vyote tangu waanze mfumo wa vyama vingi. Watu wanafanya kampeni, kura zinapigwa na vyama na wagombea binafsi wameruhusiwa kikatiba, lakini mfumo unampendelea mtawala aliye madarakani.

Katika miaka 10 yake ya kwanza madarakani, Museveni alipiga marufuku vyama vya siasa nchini humo akisema ndiyo vilikuwa mwanzo wa mgawanyiko wa mara kwa mara uliokuwa ukilikumba taifa hilo.

Hata hivyo, yeye alianzisha chama cha National Resistance Movement (NRM) kilichoanza kwanza kama vuguvugu la kisiasa na baadaye kuwa chama kamili cha kisiasa kikitokea kwenye mbavu za NRA.

Kwa sababu ya sera zake za kitaifa na uwezo mkubwa wa kioganaizesheni wa Museveni, NRM kilijikuta kuwa chama pekee chenye mizizi nchi nzima ya Uganda, huku vingine vilivyoanzishwa baada ya mwaka 1996, vikijikuta vikiwa nyuma yake.

Chama kama Democratic kilichoanzishwa na Dk. Paul Ssemogerere kilikuwa kikijulikana kwa kupendwa zaidi na watu wa kabila la Buganda, kwa mfano, na hakikuwa kinakubalika kwenye maeneo mengine au makabila mengine.

Kwa hiyo, linapokuja suala la ufuasi na mtandao, NRM ndicho chama kinachoweza kujisifu kuwa na rasilimali za kutosha kwa sababu ya kuwa chenye dola, lakini kwa mtandao mpana usiolingana na vyama vingine vinavyotaka dola.

Karibu katika kila uchaguzi, wapinzani wa Museveni wanakumbana na shuruba za vyombo vya dola vya Uganda. Dk. Kizza Besigye na sasa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ni wahanga wa mkono wa chuma wa vikosi vya ulinzi.

Kwa mujibu wa mwandishi mashuhuri wa Uganda, Andrew Mwenda, matumizi haya ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na vikosi vya ulinzi nchini humo yana faida mbili kwa Museveni.

Kwanza anacheza na akili za Waganda ambao kwa sababu ya historia yao ya nyuma, wanatamani kuwa na kiongozi imara.

Picha zozote zinazomuonyesha mtu anayetaka urais akiwa anapigwa, kunyanyaswa na kudhalilishwa, zinatoa picha kwamba mtu huyo bado hajawa tayari kuwa kiongozi wao.

Obote alitaka kuondosha tawala za kifalme za Uganda ili kujenga taifa moja lenye umoja chini yake kama kiongozi kama alivyofanya rafiki yake Nyerere Tanzania. Tatizo ni kwamba alitumia nguvu nyingi kufikia azma yake hiyo.

Katika miaka ya 1960, kwa kumtumia Idi Amin aliyekuwa mkuu wake wa majeshi, alituma wanajeshi kwenda kuvamia na kupiga watu katika makazi ya Mfalme wa Baganda; jambo ambalo watu wa kabila hawakumsamehe hadi anakwenda kaburini.

Kwa kujua hisia za Waganda kwa makabila yao, Museveni ameachia kidogo tawala za kikabila kuendelea katika sehemu kubwa ya Uganda;

Ingawa nyingi zikijiendesha kupitia ruzuku ya serikali. Matokeo yake ni kwamba watawala hawa na makabila yao hawana tatizo na utawala wa Museveni ali mradi haingilii katika mambo yao ya ndani.

Katika kitabu chake cha ‘Sowing the Mustard Seed’, Museveni anaeleza kuhusu falsafa inayoendesha maisha yake. Ameipa jina la Kayekera ikimaanisha “Constant Mobility, Constant Vigility and Constant Mistrust).

Kwamba, mara zote, hatabiriki, muangalifu na hamuamini yeyote. Pengine hii ndiyo siri yake kubwa zaidi ya kukaa madarakani kwa takribani miongo minne sasa.