TOKYO,JAPANI

WIZARA  ya elimu ya Japani inapanga kutambulisha masomo Skuli yanayolenga kuwafunza watoto jinsi ya kuzuia uhalifu wa kingono.

Maofisa wa wizara hiyo walisema skuli hazijafundisha vya kutosha kuhusu uhalifu na unyanyasaji wa kingono.

Walisema kwamba watoto wa skuli za msingi wa madarasa ya chini wakati mwengine hawaelewi kwamba wananyanyaswa.

Masomo hayo yatawafunza kutowaonesha wengine sehemu za mwili zilizofunikwa na nguo za kuogelea.

Masomo ya watoto walio katika madarasa ya juu yatafundisha kuhusu hatari zinazohusiana na mitandao ya kijamii.

Kwa wanafunzi wa sekondari ya chini na juu, masomo hayo yatajadili vurugu inayotokea baina ya wachumba na kuwaelekeza wanafunzi namna ya kuepuka kuwa waathiriwa au wanyanyasaji.

Kadhalika Wizara hiyo inapanga kuanza masomo ya majaribio katika manispaa chache kuanzia mwaka wa masomo unaoanza mwezi Aprili mwakani.

Inapanga kutambulisha masomo hayo nchini kote mwaka 2023 baada ya kuandaa nyenzo na miongozo ya kufundishia.