NA MWAJUMA JUMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, amewataka wananchi kuwa wabunifu ili kufanikisha utekelezwaji wa dhana ya uchumi wa buluu.

Alisema dhana hiyo hutumiwa zaidi na nchi za visiwa na zinazopakana na bahari, husaidia kuimarisha uchumi kutokana na udogo wa ardhi ambayo inahitajika kwa mambo mbali mbali.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka saba ya Mfuko wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi alisema mipango na mikakati ya Serikali ukiwemo dira ya Zanzibar ya 2020/2025 na mpango wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini (MKUZA) na sera mbali mbali inajielekeza katika kubadilisha hadhi ya Zanzibar kwa kuwa na uchumi endelevu na unaojitegemea.

Hivyo alisema kuwa hatua hiyo inahitaji nguvu za pamoja, kuaminiana, nidhamu na uadilifu. Ili kuweza kufikia malengo hayo ya serikali.

Aidha waziri Soraga alisema uchumi wa buluu una faida kubwa na mambo mengi miongoni mwa hayo ni mazao yatokanayo na mwani na mazao mengne ikijumuisha shughuli za utalii.

Aidha alisema; “Kuna taarifa ambazo si za kufurahisha kuwa asilimia 90 ya biashara mpya zinazokufa hutokana na utumiaji wa fedha za mtaji tofauti na malengo yake, tujirekebishe na tatizo hilo ili tusipoteze fursa”.

Sambamba na hayo waziri huyo aliahidi kuwa serikali itaendeleza hatua hiyo iliyofikiwa na kushirikisha makundi yote kama ambavyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi alivyoeleza kila mara katika hotuba zake.

Mapema Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mauwa Makame Rajab, alisema serikali ya awamu saba iliunda mfuko huo kwa dhamira ya kuhakikisha kila mwananchi wa Zanzibar anakuwa na shughuli halali itakayompatia kipato ili kukidhi mahitaji yake ya maisha yake, familia na ikiwezekana kuchangia katika uchumi wa taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mfuko huo Suleiman Ali Haji, alisema uwepo wa mfuko huo kumewawezesha wanawake kushiriki katika shughuli mbali mbali za uzalishaji mali na hivyo kujiongezea kipato.

Alisema kwa ajili hiyo hata mtazamo wa wanawake sasa umebadilika kutoka kuwa wa kijamii pekee na kuwa wa kiuchumi.

Alifahamisha kwamba uamuzi wa wanawake kuchukua mikopo kumesababisha kuwa na maamuzi sawa kati ya wanaume na wanawake ambapo zamani masuala ya mikopo yalikuwa yakiamuliwa na kuratibiwa na wanaume.

Mfuko wa uwezeshaji ulianzishwa mwaka 2013 ambapo hadi kufikia Novemba mwaka huu, jumla ya mikopo 3,628 yenye thamani ya shilingi 4,555,798,000 imetolewa Unguja na Pemba.