NA MARYAM SALUM

WATENDAJI wa serikali, wametakiwa kuacha  kufanyakazi kwa mazoea na badala yake wabadilike ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya nane.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soroga, alisema azma ya serikali ni kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika taasisi zake.

Alisema kila mfanyakazi lazima awe na mpango mkakati  wake utakaomuwezesha kufanyakazi zake kwa lengo la kuleta tija kwa jamii.

Alifahamisha kuwa watendaji wa wizara hiyo waelewe kuwa wana jukumu kubwa la kuhakikisha dhamira ya uchumi na uwekezaji unaleta tija kwa jamii yote.

Alitoa wito kwa watendaji wakiwemo wakurugenzi,wakuu wa vitengo na maofisa wadhamini pale wanapopewa wazo na watendaji wao wasipuuze na badala yake walifanyiekazi kwa maslahi ya umma.

Alisema serikali ya awamu ya nane ipo karibu na wananchi katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa ajili ya wananchi wote.

Aliwataka wakuu wa idara zilizomo ndani ya wizara hiyo
kuondokana na ubaguzi hasa katika ajira zinapotokea ili kuepusha lawama zisizokuwa na lazima.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mauwa Makame Rajab, aliwataka wafanyakazi hao kujitambua kwa kuacha kufanyakazi kwa mazoea.

Nae Ofisa Mdhamini wa wizara hiyo, Hakimu Vuai Shein, alisema atahakikisha anatoa ushirikiano kwa waziri huyo ili anatekeleze majukumu yake vizuri.