NA MWAJUMA JUMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, amewataka wananchi kuwa wabunifu kufikia uchumi wa buluu ambao zaidi hutumiwa na nchi za visiwa kutokana na uchache wa ardhi.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka saba ya Mfuko wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi, alisema mipango na mikakati mikuu ya Serikali, ikiwepo dira ya Zanzibar ya 2020/2025 na mpango wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini pamoja na sera mbali mbali, inajielekeza katika kubadilisha hadhi kuwa na uchumi endelevu na unaojitegemea.

 “Mafanikio mliyonayo na yanayokuja kwa kasi ya awamu ya nane yatategemea na nyinyi pia, hivyo pamoja na mafanikio hayo mliyoyapata napenda kuwakumbusha nyinyi nyote wajasiriamali kuendelea kutumia fedha zenu za mikopo na mitaji maalumu muliyoomba ili mfikie matarajio”, alisema.

Aidha alisema “Kuna taarifa ambazo si za kufurahisha kuwa asilimia 90 ya biashara zote mpya zinazokufa hutokana na utumiaji wa fedha za mtaji tofauti na malengo yake, tujirekebishe na tatizo hilo ili tusipoteze fursa”.

 “Kama nunavyofahamu kutokana na juhudi kubwa za viongozi wetu wa serikali zote mbili Tanzania imefikia uchumi wa kati, hatua hii ni kubwa na inayostahiki pongezi za dhati na za kipekee”, alisema.

Sambamba na hayo Waziri huyo, aliahidi kuwa Serikali ya awamu ya nane itaendeleza hatua hiyo iliyofikiwa na kushirikisha makundi yote kama ambavyo Rais Hussein Ali Mwinyi alivyoeleza kila mara katika hotuba zake.

Mapema Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mauwa Makame Rajab, alisema serikali ya awamu saba iliunda mfuko huo kwa dhamira ya kuhakikisha kila mwananchi wa Zanzibar, anakuwa na shughuli halali itakayompatia kipato, ili aweze kukidhi mahitaji yake ya maisha yake, familia na ikiwezekana kuchangia katika uchumi wa taifa.

Hivyo alisema, kuwa jambo hilo limekuwa ni la manufaa kwa taifa na limewaokowa akinamama na kina baba wengi pamoja na vijana.

“Mfuko huu umetengeneza ajira nyingi, umewafumbuwa macho watu wengi na kuwafanya wawe wajasiriamali pamoja na kusaidia vikundi mbali mbali vyao wenyewe vinavyoendeleza shughuli zao mbali mbali ambazo zilianzishwa kutokana na mfuko huo.