KHARTOUM,SUDAN

JESHI la Sudan limeripoti kutokea mashambulizi ya mpakani kati yake na jeshi la Ethiopia na wanajeshi wake kadhaa kuuwawa,katika hatua ambayo inaweza kusababisha uhasama baina ya mataifa hayo mawili jirani.

Taarifa hiyo ya jeshi inasema shambulizi lilitokea wakati kikosi kikitoka katika doria jimboni al-Qadarif, lililopo katika mpaka wa Ethiopia.

Hata hivyo taarifa hiyo haijataja wanajeshi wangapi waliuwawa au kujeruhiwa.

Lakini maofisa wa jeshi tofauti ambao walizungumza kwa masharti kutotajwa majina yao walisema katika mapambano hayo wanajeshi wanne akiwemo mwenye cheo cha meja, waliuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Walisema jeshi lilipeleka vikosi katika eneo la mpaka. Baada ya kuzuka kwa mapigano ya ndani mwezi uliopita nchini Ethiopia katika jimbo la Tigray, Sudan ilipeleka kwa ulinzi wake wanajeshi 6,000 katika eneo la mpakani.