ZAGREB,CROATIA

TETEMEKO kubwa la ardhi limelikumba eneo la katikati mwa Croatia na kusababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine wasiopungua 26.

Shirika la Marekani la Utafiti wa Kijiolojia linasema tetemeko hilo lilitokea Jumanne majira ya mchana kwa saa za Croatia na lilikuwa na ukubwa unaokadiriwa kuwa 6.4 kwenye kipimo cha Richter na kina chake kilikuwa kilomita 10.

Maofisa wa Serikali ya Croatia walisema majengo mengi yalianguka katika mji uliloathirika zaidi wa Petrinja.

Walisema msichana wa umri wa miaka 12 alifariki katika eneo hilo, na wengine watano walifariki jirani na mji huo.

Waziri Mkuu Andrej Plenkovic aliwahi katika eneo palipotokea janga hilo. Alisema wanajeshi wa nchi hiyo walipelekwa kusaidia operesheni za utafutaji na uokozi.

Tetemeko hilo pia lilisikika katika mji mkuu wa nchi hiyo Zagreb, takribani kilomita 50 kutoka kwenye kiini chake. Picha za video kutoka jijini humo zinawaonyesha watu wakikimbilia mitaani.

Mji wa Zagreb bado unarejea hali ya kawaida kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililotokea mwezi Machi ambalo pia lilisababisha vifo.