MANILA,UFILIPINO

TETEMEKO la ardhi lenye ukubwa wa 6.3 kwa vipimo vya Richter limeyapiga maeneo kadhaa ya Ufilipino kwenye Siku ya Krismasi.

Wakaazi kwenye mji mkuu, Manila, waliripoti mtikisiko wa majengo,huku mipasuko ikiripotiwa kwenye jimbo la Batangas katika kisiwa kikuu cha Luzon, likienda umbali wa kilomita 114 chini ya ardhi.

Shirika la Utafiti wa Miamba la Marekani limesema tetemeko hilo limetoka majira ya saa moja na dakika 43 asubuhi.

Katika mji wa pwani wa Calatagan, umbali wa kilomita 90 kusini mwa mji mkuu Manila, polisi inasema licha ya tetemeko kupiga kwa muda mfupi, hakukuwa na madhara yoyote.

Visiwa vya Ufilipino viko kwenye duara la moto katika Bahari ya Pasifiki, sehemu ambayo inakumbwa mara kwa mara na matetemeko ya ardhi.