ZANZIBAR ni nchi yenye historia kubwa, lakini pamoja na sifa zote nzuri ambazo visiwa vyetu vimejaaliwa kuwa nazo tuna tatizo la muda mrefu la kuzagaa uchafu.

Uchafu wa taka zilizozagaa maeneo mbalimbali, zilizoshindwa kuzolewa katika maeneo rasmi na hata wakati mwengine makari kutiririsha maji yenye harufu mbaya ni jambo linalotia doa taswira n ahata ustaarau wetu.

Wakati mwengine huwa tunajiuliza tumefikwa na balaa gani kiasi kwamba kila mwaka lazima kutokee maradhi ya mripuko ya kipindupindu, kumbe tatizo ni uchafu.

Uchafu uliooenea katika maeneo ya miji ya Zanzibar haushwi kutoa mbinguni ama wanyama ambao hawakuwa uwezo mkubwa wa akili kwamba wao ndio wanaosababisha.

Uchafu katika mji yetu unazalishwa na mikono yetu wenyewe sisi wakaazi wa miji ambao tunaelezwa kwamba Mwenyezi Mungu ametupa akili na maarifa ya kupambanua zuri na baya.

Labda tuseme tu kwa bahati mbaya sana akili zetu tulizopewa zimeshindwa kufikiri kuona ubaya wa uchafu, ndio maana hatuoni kama kuzagaa kwa uchafu hilo ni tatizo.

Kiukweli usafi ni jambo ambalo mtu mwenye akili timamu aliyejaaliwa maarifa na ufikiri mzuri wa kiutu uzima, anapaswa kufahamu umuhimu wake kufanya kuwa sehemu ya utamaduni wa maisha yake.

Tunaelewa manispaa na mabaraza ya mji ndiyo yaliyopewa dhamana ya kusimamia suala usafi, hasa ikizingatiwa kuwa wao ndio wanaokusanya mapato ya kutekeleza kwa ujumla suala la usafi.

Hata hivyo fedha wanachukua kila mwezi, lakini tatizo la taka kuzagaa ovyo na hata zile zilizofikishwa kwenye majaa rasmi hushindwa kuzolewa, hapa ndipo unapojiuliza masuali mengi fedha zinazokusanywa zinakwenda wapi? Na zinatumika vipi?

Kwa upande mwengine kuna wananchi ambao wamekosa elimu ya usafi wa mazingira wanachojua wao wapo mjini kwa hiyo muhimu kuoga na kunyoosha nguo kwa pasi.