NA ZAINAB ATUPAE
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya KMKM Ame Msim, amesema wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo dhidi ya Mlandege utakaochezwa baadae wiki hii.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema wanaamini kuwa mchezo huo utakaopigwa Disemba 25 mwaka huu, utakuwa mgumu lakini hawana wasiwasi nao.
Alisema mechi hiyo itakuwa ngumu ikizingatiwa kuwa wanacheza na timu inayotetea ubingwa wake ilioupata msimu uliopita.
Alisema kila mmoja anahitaji pointi tatu,ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.
“Tunazitaka pointi kwa hiyo tunahakikisha tunapambana kwa kila hali kupata nafasi hiyo,” alisema.
Hivyo alisema anaamini kuwa watafanya vyema na kushina mechi kutokana na kuwa timu yake ipo vizuri kwa kila nafasi.
Alisema kwa kushirikiana na makocha wenzake wataendelea kutoa mazoezi na kurekebisha makosa yalijitokeza katika mechi walizo cheza.
“Kuna kasoro ambazo zilijitokeza kwenye mechi tulizocheza,lakini tunazirekebisha na naamini kila tukienda mbele zitaondoka,”alisema.
Aidha aliwataka wachezaji kuwa kitu kimoja na viongozi wao na kufuata ambacho wanafundishwa kwa lengo la kuleta ushindi kwenye mechi zao ambazo wanacheza.
“Tunamalengo mengi,lakini kwanza cha muhimu nikushinda kila mechi hatua kwa hatua,”alisema.
Katika msimu huu wa ligi, mabingwa hao wa zamani, imecheza michezo mitano, imeshinda minne na kupoteza mmoja ikiwa kileleni kwa ligi hiyo na pointi 12 mkononi.