NA KHAMISUU ABDALLAH

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, limeeleza kuwa limeweka mpango madhubuti ili kuhakikisha wanawazuia uhalifu mkaoani humo katika kipindi chote cha sikukuu ya krismas na mwaka mpya.

Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Awadh Juma Haji, aliyasema hayo wakati akitoa taarfa kwa vyombo vya habari ofisini kwake Mwembe Madema jana.

Alisema wahalifu hutumia siku hizo kufanya uhalifu ukiwemo wa kuwapokonya mali zao wananchi, hivyo jeshi litakuwa macho wakati wote ili kuona wananchi wanasherehekea sikukuu hizo katika hali ya usalama.

Kamanda Awadh alibainisha kwamba wataimarisaha ulinzi katika maeneo yote ikiwemo katika nyumba za ibada kwa kuweka askari waliovaa sare, kiraia na kufanya doria kwa gari na kikosi cha mbwa na farasi katika sehemu zote za fukwe na viwanja vya sherehe.

Alisema lengo la doria hizo ni kuhakikisha inadhibiti wahalifu wote wanaotumia mwanya wa sikukuu katika kuendeleza vitendo vya kihalifu ikiwemo uporaji na unyanganyi wa kutumia nguvu.    

Alisema lengo la jeshi hilo ni kuhakikisha amani na utulivu inaendelea kudumu katika kipindi chote cha sikukuu hizo na kuona wananchi wanamaliza mwaka wa 2020 kwa salama na amani.

Akizungumzia siku ya mkesha wa mwaka mpya, alisema jeshi lake litaweka ulinzi katika maeneo yote ikiwemo viwanja vya watoto na fukwe za bahari.

Mbali na hayo Kamanda Awadh, aliwaomba wazazi na walezi kutowaachia watoto wao wadogo kwenda peke yao katika viwanja vya kusherehekea sikukuu kwani uzoefu unaonesha kwamba kipindi hicho matukio mengi ya unyanyasaji na vitendo vya udhalilishaji hujitokeza kwa wingi.

“Tumejipanga kwa hali zote na hatutosita kumchukulia hatua mtu yoyote atakaehusika na vitendo hivyo na vyengine vya vya uvunjifu wa amani,” alieleza akamada Awadh.

Aidha aliwataka wamiliki wa kumbi za starehe zilizomo katika mkoa wa Mjini Magharibi kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu zilizowekwa katika kuendesha shughuli hizo na kufuata muda kufunga kumbi zao saa 6:00 usiku.

Akizungumzia usalama barabarani alisema jeshi la polisi litaweka vizuizi vya barabarani ili kukagua vyombo vya moto vinavyoingia na kutoka ndani ya mkoa huo.

Awadh pia alitumia muda huo kuwataka madereva wa vyombo vya moto vikiwemo vyombo vya maringi mawili na watumiaji wengine wa barabara kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

“Tunatoa onyo kwa madereva waache kuendesha vyombo vyao wakiwa wamelewa, kupiga misere, kuendesha vyombo vyao kwa mwendo kasi kwani kufanya ni kosa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Kwa upande wa wananchi aliwaomba kuzingatia muda katika kutumia maeneo mbalimbali ya fukwe na kuona wanarudi nyumbani kwa salama.

Hivyo alisisitiza kuwa jeshi lake litaendelea kufanya doria na misako katika maeneo mbalimbali ya mkoa wake na kuwataka wananchi kushirikiana na jeshi lao katika kuwafichua wahalifu na kuona wanachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Sambamba na hayo alisema jeshi halitakuwa na muhali kwa mtu yoyote ataejihusisha na vitendo vya uvunjaji wa sheria katika kipindi chote cha sikukuu na baada ya skukuu.