HIVI karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alifanya ziara ya siku mbili kisiwani Pemba, ambapo ziara hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya kuwapa shukrani wananchi wa mikoa miwili ya kisiwa hicho.

Shukrani alizokwenda kuwapa wananchi hao ni kwa hatua yao ya kufanikisha Chama cha Mapinduzi kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika ziara hiyo, shukrani za Dk. Mwinyi hazikuishia kwa wananchi na wanaCCM pekee, pia alizielekeza kwa kukutana na makundi mbalimbali ya jamii ambayo kabla ya uchaguzi kwa maana ya wakati wa kampeni alikutana nao kuwaomba kura.

Kwa hakika kitendo kilichofanywa na Dk. Mwinyi kwenda kisiwani Pemba pamoja na maeneo mengi ya Zanzibar kukutana na wadau muhimu waliofanikisha ushindi, hii ni moja ya tabia ya mtu anayeweza kuitwa muungwana.

Kwa kawaida mtu asiye muungwana anapofanyiwa jambo la hisani huwa hakumbuki na kama atakumbuka basi hatojali thamani ama uzito wa jambo alilofanyiwa.

Lakini imekuwa kinyume sana kwa Dk. Mwinyi ambaye kutokana na uungwana na imani aliyojaaliwa nayo, amekumbuka kukutana na wadu ambao Oktoba 28 mwaka huu walitumia muda na hata gharama bila ya kushindikizwa kwenda kupiga kura.

Katika hotuba alizozitoa akiwa kisiwani Pemba kwenye ziara hiyo mahususi ya shukrani, kwa hakika zimebeba ujumbe mzito unaonesha msisitizo wa kutokubaliana na vitendo vya wizi na ufisadi kwenye taasisi za umma.

Katika moja ya mkutano wake alisikika akiwataka wananchi wamvumilie kwa sababu anakusudia kufanya maamuzi magumu dhidi ya waliohusika kujihusisha na vitendo vya ufisadi na wizi wa mali za umma.

Sisi kama wananchi kwa hakika Dk. Mwinyi tunakupa pongezi maalum kwa sababu tuelewa fika vita dhidi ya rushwa, wizi na ufisadi vinahitaji jemedari jasiri ambaye sio atakataa tu kwa maneno bali pia atatekeleza kwa vitendo.

Wazanzibari kwa muda mrefu nyuma tumeimbishwa na viongozi wetu rushwa adui wa haki, kwa bahati nzuri wimbo huo ulizoeleka katika ndimi zetu na tukaamini waliokuwa wakituimbisha ambao viongozi wetu nao watakuwa sio wanatueleza bali watasimamia kupiga vita.

Kumbe mambo yalikuwa kinyume kabisa mchana kwenye muangaza wa jua kali baadhi ya viongozi wanatwambia rushwa adui wa haki, lakini wakiingia gizani wanachota kama vile fedha wanazojikusanyia hazina mwenyewe.

Dk. Mwinyi suala la rushwa na ufisadi sio linakukera peke yako, bali sehemu kubwa ya jamii limewafika shingoni kwa sababu fedha wanazochota mafisadi ni miongoni mwa kodi tunazokatwa ama mipoko ya nje ambayo baadae tutalazimika kuilipa.

Kwa sababu wewe kiongozi wetu tunakubaliana na wewe unaposema hutafukua makaburi wala kumtafuta mchawi, lakini kama kuna makaburi machache ambayo yana ushahidi muhimu ambao tunapaswa kuujua kujua maiti aliyekuwemo si vibaya kama utafukua.

Pamoja na yote hayo, tutakuvumilia kama ulivyotuomba, lakini pia tunakuona unachelewa kwa sababu baadhi ya mafisadi wanatafuta njia za kuficha kile walichopora ili watumie kwa raha na familia zao.

Pamoja na kukupongeza kuonesha udhati wa kupambana na rushwa, tukuhakikishie Dk. Mwinyi una jeshi kubwa la kufanikisha ushindi kweny vita dhidi ya rushwa jeshi hilo kama hulijuia ni imani kubwa ya wananchi walionyuma yako.