KATIKA hotuba zake mbalimbali alizopata kuhutubia, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alibainisha wazi kuwa yupo tayari kuendeleza maridhiano.

Ikiwa zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu serikali mpya ya awamu ya nane iingine madarakani, upande wa ulioshindwa kwenye uchaguzi ulikuwa unatathimini kauli ya Dk. Hussein Mwinyi juu ya mariadhiano.

Dk. Mwinyi aliendelea kusisitiza msimamo wake kwamba yupo tayari kuendeleza maridhiano ya kisiasa ambayo yatawaleta pamoja wanzanzibari wote kwa ajili ya kuijenga nchi yao.

Wakati analitangaza baraza la mawaziri lenye wizara 15, Dk. Mwinyi aliziacha nafasi mbili ambapo alieleza wazi wizara hizo zipo wazi endapo chama kilichopata nafasi ya pili kwenye uchaguzi mkuu kipo tayari kujiunga kwenye serikali.

Dk. Mwinyi aliziacha nafasi hizo ili kuupa nafasi upinzani kujiunga na serikali ya umoja wa kitaifa, lakini pia hilo lina takwa la katiba ya Zanzibar lililotokana na marekebisho ya 10.

Kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza kwamba muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia.

Kwa muda wote upinzani ulikuwa unajadili ukubali ama usikubali kujiunga na serikali ya umoja, Dk. Mwinyi aliendelea kuwasubiri hadi wafikie muafaka na kwa ridhaa yao wakapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Kwa bahati nzuri jina lililotolewa ni la mwanasiasa maarufu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye baada ya kuapishwa anarejea kwa mara nyengine tena kushika nafasi hiyo.

Tahariri yetu inataka kutoa pongezi za dhati kwa Rais wa Zanzibar na Mwneyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi kwa kutekeleza dhamira yake aliyoahidi kwamba ataendeleza maridhiano ya kisiasa.

Waswahili walisema nyota njema huonekana alfajiri, bila shaka huu ni mwanzo wa mengi yenye manufaa ambayo wazanzibari tutanufaika nayo chini ya uongozi wa rais wetu huyo.