TANGU ilipoundwa Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA), takriban miaka minane iliyopita hatukuwa tukiona mamlaka hiyo ikitekeleza majukumu yake kama matarajio ya wengi walivyotegemea.
Kila tunaposikia mamlaka inayofanana na hiyo upande wa pili wa muungano inavyotekeleza majukumu yake, masuali yetu mwengi yalikuwa ZAECA yetu inashindwa nini?
Tulikuwa tukishangazwa sana kwanini Zanzibar imechukua hatua za kuunda mamlaka hiyo wakati hatuoni malalamiko ya rushwa yanayotolewa na wananchi yanafanyiwa kazi.
Lakini cha kushangaza zaidi hata watuhumiwa wa rushwa na ufisadi katika taasisi mbalimbali za umma wanaendelea na majukumu yao kama kawaida na kama vile hakuna malalamiko.
Hatuwalaumu sana ZAECA pengine mazingira ya uhuru wa kutekeleza majukumu yao ili wananchi waone matokeo chanya ulibanwa pengine na mifumo iliyokuwepo.
Tunaposema wazanzibari sote ndugu huwa tuko kwenye usahihi kabisa mkubwa, pengine watuhumiwa wengi wa rushwa na uhujumu wa uchumi ni ndugu ama jamaa za wakubwa.
Kwa hiyo kila unayemgusa kwa tuhuma za rushwa ndio yale aliyesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi mtoto wa mkubwa, ndugu yake fulani ama mke wa fulani.
Pamoja na hayo kwa sababu ZAECA ni taasisi ya Zanzibar watu ambao tunasifika kuwa taia ya muhali tabia ya kutoambizana ukweli, nayo pengine ilijikuta kwenye hali kama hiyo.
Lakini ukweli ni kwamba ili nchi iwe na dhamira ya kupiga vita rushwa na uhujumu uchumi, lazima pawepo na dhamira ama nia njema kutoka kwa viongozi wa kisiasa ‘political will’.
Haiwezekani wananchi wa hali ya chini wanaopapatua mlo mmoja kwa siku wanaambiwa rushwa adui wa haki, lakini kiongozi ndiye anayetajwa kuhusika rushwa kwenye maeneo mbalimbali na kila kwenye mradi ana ‘ten percent’.
Wakari mwengine huwa tunashangaa sana, hivi wewe kiongozi serikali inakulipa mshahara mkubwa unaotesheleza na kuzidi mahitaji yako ya mwezi mzima, lakini wewe ndiye mkubwa wa kula rushwa na kuhujumu uchumi je anayelipwa mshahara wa shilingi 350,000 yeye afanyeje?
Ni vigumu kuukubali ukweli, lakini ili twende inavyotakiwa lazima tuambizane ukweli, kiongozi anaposimama kusema rushwa ni adui wa haki, asiishie tu kulitamka neno hilo mdomoni mwake bali atekeleze kwa vitendo na aishi nalo katika maisha yake ya kila siku.
Kiongozi anapofanya hivyo atakuwa ameonesha imani na atakuwa mfano wa kwa jamii, lakini vyenginevyo vita hivi vitakuwa vigumu mno.
Kama serikali ya awamu ya nane imeipa meno ZAECA tungependa kuwaona wanafunguka na kutanua kikosi chao kipana katika kuhakikisha wanapambana na rushwa na uhujumu wa uchumi.
Tunadhani tatizo la utashi wa kisiasa ‘political will’ katika vita dhidi ya rushwa na uhujumu wa uchumi hivi sasa halina tatizo, tungependa kuiona ZECA inaongeza nguvu na mikakati.
ZAECA tunataka kuwaona waking’ata na sio vyenginevyo, tukiamini kuwa wananchi wapo tayari kuwasaidia.