NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliajina Maliasili Dk. Soud Nahoda amesema serikali ya awamu ya nane itaendelea kuunga mkono juhudi za ubunifu wa miradi wa wajasiriamali ili wafikie malengo waliyojiwekea.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wajasiriamali wa kiwanda cha kusarifu mazao cha Mtule AMKOS kilichopo Paje, mkoa wa Kusini, Unguja.

Alisema lengo la serikali ni kuona wananchi wa Zanzibar wanakuwa wabunifu na uwezo wa kuibua miradi ili wajiajiri wenyewe na kuondokana na utegemezi.

Aidha alisema iwapo wananchi watakuwa na mwamko pamoja na kufuata maelekezo ya viongozi wao katika suala la uimarishaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii itasaidia kutimiza azma na mipango ya mabadiliko ya maendeleo yaliokusudiwa na serikali.

Waziri huyo alisema, serikali imeandaa mikakati na mipango imara yenye manufaa kwa wajasiriamali ikiwa ni pamoja na kuwakopesha mitaji isiyo na riba.

Pamoja na hayo waziri huyo aliwaahidi wajasiriamali hao kutatua changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kupatiwa fursa za kutangaza bidhaa zao katika masoko yao ndani na nje ya Zanzibar.

“Jambo la msingi kwa wajasiriamali wote nchini kuhakikisha manafuata taratibu na maelekezo ya wataalamu ili muweze kuingia katika ushindani wa kibiashara,” aliongeza Dk. Soud.

Mapema Mjumbe wa Bodi ya Kiwanda cha Mtule AMKOS, Mohamed Haji Ameir, alisema pamoja na mafanikio waliyonayo, wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha wa kununua vitendea kazi kama vile vifungashio.

Alifahamisha kwamba pamoja na changamoto hizo zimepelekea hadi sasa bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo ikiwemo ya ‘tomato paste’ kutokubalika katika soko la utalii ambako kuna mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo.