MABADILIKO ya tabia nchi ni miongoni mwa changamoto kubwa inayoyakabili maneo mbali mbali ya visiwa vya Zanzibar, hususan yale yalio kando ya fukwe za bahari.

Maeneo husan kisiwani Pemba yaliyokuwa yakitumiwa kwa ajili ya kilimo yamekumbwa na uvamizi ma maji ya bahari, hivyo kifanya shughuli ya kilimo katika maeneo hayo kuwa vigumu kuendelea.

Wataalamu wa masuala ya mazingira wanaeleza kuwa kupanda kwa maji ya bahari kunakotokana na kuongezeka kwa kiwango cha joto baharini.

Kupanda kwa kiwango hicho cha joto kumesababisha maeneo ambayo yalikuwa na baridi sana kiasi cha kuwepo mapande makubwa ya barafu kuyuka na hivyo kina cha maji ya bahari kuongezeka.

Tafiti mbalimbali za kitaalamu zimethibitisha kuwa ongezeko la joto linatokana na shughuli za binaadamu hasa viwanda kuzalisha kiwango kikubwa cha gesi chafu.

Hivyo kadiri nchi zinavyozalisha gesi chafu ndivyo hali ya joto inavyoongezeka, ambapo kwa bahati mbaya athari za tabia nchi huyakumba hata mataifa ambayo hayana viwanda vyenye kuzalisha gesi chafu.

Tatizo jengine ni kwamba hayo mataifa yenye kuzalisha gesi chafu zenye kuongeza kiwango cha joto duniani yanavutana katika utekelezaji wa mikataba waliyojiwekea ya kuzuia uzalishaji wa gesi chafu.

Hata pale athari za moja kwa moja zinapojitokeza kwa mataifa masikini, hawasaidi ndio mana hivi sasa sehemu mbalimbali ulimwneguni kunashuhudiwa mabadiliko ya miongo.

Athari za mabadiliko ya miongo zimesababisha majanga makubwa yakiwemo mafuriko, vimbunga na hata baadhi ya sehemu kukubwa na ukame.

Athari hizo pia zimekuwa zikishuhudiwa katika maeneo ya baharini, hasa kuharibika kwa matumbawe kutokana na ongezeko la joto.

Zanzibar kama nchi, haipaswi kukaa nyuma kusubiri ushahidi wa athari zaidi za mabadiliko ya tabia nchi, bali kitu cha msingi ni kuhakikisha jamii inahamaishwa katika kukabiliana na hali hiyo.

Tuwahimize wananchi wetu wahakikishe wanapanda miti, ambayo kwanza husaidia kunyonya gesi chafu, lakini pia miti huwa chanzo cha mvua.

Tunavyoamini tunaweza kuziepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi kama kila mmoja atawajibika katika kuzuia janga hilo huku tukiwachukulia hatua wale wanaokata miti bila ya sababu za msingi.