NA TATU MAKAME

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema itafanya kila jitihada kuhakikisha jengo la Beit Al Ajaib, linarudi kama lilivyokuwa awali na kuendelea kuwa nembo ya Mji Mkongwe.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Lela Muhamed Mussa, alisema hayo kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusiana na kuanguka kwa jengo hilo Disemba 25 mwaka huu.

Alisema serikali kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya kale imeunda Tume maalum ya uchunguzi, kuchunguza kadhia nzima ya kuporomoka kwa jengo la Beit Al Ajaib na kubaini kila kilichotokea  pamoja na kuishauri  serikali hatua mbalimbali zinazostahiki kuchukuliwa kutokana na  yatakayobainika  kwenye uchunguzi huo.

Aliwahakikishia Wazanzibari, Watanzania na dunia kwamba serikali itafanya   jitihada zake zote ikiwa wenyewe binafsi au kwa msaada wa wahisani  kuhakikisha jengo linarudi katika hali yake ya awali baada ya kufanyiwa ukarabati.

Hata hivyo aliwasisitiza wananchi kuzidi kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu, kwani hatua stahiki zinaendelea ili kubaini chanzo cha kuporomoka kwa jengo.

“Tunawaomba wananchi mutulie pindi ikibainika kuwa kuna uzembe au hujuma kwa mtu au taasisi yoyote iliyopelekea maafa hayo hatua zitachukuliwa”, alisema Waziri huyo.

Hata hivyo alisema serikali inatoa pole kwa wananchi   wote wa Zanzibar kutokana na hasara iliyosababishwa na ajali hio, pia inatoa pole kwa familia za wahanga wawili waliopoteza maisha katika eneo la ajali na maiti zao zilipatikana usiku wakati zoezi la uokozi lilipokua likiendelea kufanyiwa ukarabati.

Aidha Waziri lela alibainisha kwamba majeruhi wanne ambao ni wafanyakazi waliopata majeruhi katika eneo la ajali na watu wote waliopata athari yoyote iliyosababisha na kadhia hiyo kuwa nao bega kwa bega katika kipindi hichi kigumu cha msiba na kuuguza.

Aidha alisema serikali inatoa pole kwa  kuathirika  Nembo ya urithi wa Dunia iliyopo ndani ya Mji  Mkongwe wa Zanzibar kutokana na kuporomoka  kwa sehemu  ya mbele  ya jengo  hilo ambalo ni urithi wa dunia.

Jengo la Beit Al Ajaib liliopo Rofodhani Mjini Zanzibar liliporomoka  sehemu ya mbele ya upande wa kulia  wakati shughuli za kufanyika  matengenezo makubwa zikiendelea  ambazo zinafanywa na mkandarasi  kutoka nchi  ya Italia aitwae ‘Construzioni Generali Gilardi S.P.A ( CGG)’ kwa ufadhili wa Serikali  ya Ufalme wa Oman kwa gharama ya Dola za Kimarekani takriban milioni 5.6.