NAIROBI,KENYA

UCHAGUZI mdogo wa Ugavana kwenye Kaunti ya Niarobi utafanyika Februari tarehe 18 mwakani.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alivitaka vyama vyote vya kisiasa vyenye nia ya kushiriki uchaguzi huo kuwasilisha majina ya wagombea wake ifikiapo Disemba tarehe 28 mwaka huu.

Aidha wagombea binafsi walishauriwa kuwasilisha majina yao kwa IEBC na nembo watakazotumia ifikiapo siku hiyo ya Jumatatu.

Kulingana na IEBC kampeni za uchaguzi huo zitafanyika kati ya Januari tarehe 18 hadi Februari tarehe 15 kati ya saa moja asubuhi na saa kumi na mbili jioni.

Uchaguzi huu mdogo unatokana na kuondolewa kwa aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kutokana na tuhuma mbalimbali ukiwemo ufisadi.

Ikumbukwe Sonko aliwasilisha kesi mahakamani akitaka shughuli ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo isitishwe,Sonko alisema yuko tayari kujitetea mahakamani.

Sonko aliendeela kuwashtumu maseneta kwa kukubali hoja ya kumtimua madarakani akidai  hatua hiyo ilichochewa na misimamo yake mikali dhidi ya serikali.

Tayari wanasiasa mbalimbali walitangaza nia ya kuwania ugavana jijini Nairobi.