KAMPALA, UGANDA

UGANDA imewasilisha ombi la kupata chanjo ya covid19 kama inavyotakiwa na COVAX facility.

Wizara ya Afya nchini Uganda imethibitisha kuwasilisha ombi hilo na kupatiwa chanjo iliyovumbuliwa hivi karibuni ya kukabiliana na ugonjwa wa corona.

Ombi hilo limetumwa wakati maambukizi ya virusi vya corona nchini humo yakizidi kupanda kwa kasi huku baadhi ya wanasiasa wakituhumiwa kusambaza virusi vya corona kutokana na muingiliano wa watu katika kampeni za kisiasa zinazoendelea.

Maneja wa mipango ya taifa ya upanuzi wa chanjo katika wizara ya afya nchini Uganda, Alfred Driwale alisema kuwa wameanza mchakato huo kwa majuma mawili na wamewasilisha ombi la kupatiwa chanjo hiyo.

Dk. Driwale aliongeza kwamba chanjo hiyo watapewa watu waliomstari wa mbele katika kupambana na virusi vya corona pamoja na watu walio hatarini kuambukizwa virusi vya covid19.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO), COVAX tayari imeshirikisha mataifa 186 duniani kati hayo 47 ni kutoka bara la Afrika.

Uganda ikiwa moja ya mataifa ya uchumi wa chini yanayokwenda kunufaika kutoka kwa COVAX Facility. Kufikia sasa hakuna chanjo iliochaguliwa kutumiwa katika mataifa, isipokuwa kuna maendeleo na matarajio ya majaribio ya chanjo ya corona kila siku kwa wanachama wa COVAX Facility.