LONDON, UINGEREZA

MAMLAKA nchini Uingereza zimeongeza maeneo zaidi yaliyowekewa sheria kali za virusi vipya vya corona kuanzia jana kutokana na aina mpya ya virusi vya ugonjwa huo kuenea kwa kasi.

Karibu asilimia 80 ya watu wote Uingereza wataguswa na hatua kali zilizochukuliwa na serikali katika kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo vipya vinavyosababisha ugonjwa wa corona.

Maambukizi yaliyosababishwa na aina mpya virusi inayoambukiza kwa kasi kuliko ile ya awali, yalirekodiwa hasa kusini mashariki mwa Uingereza, ukiwemo mji wa London.

Sheria kali ziliwekwa katika maeneo hayo huku maduka yasiyouza mahitaji ya lazima yakifungwa na watu kutakiwa kukaa nyumbani.

Hata hivyo, visa vipya vya maambukizi ya siku zaidi ya 50,000 viliripotiwa nchini Uingereza Jumanne na Jumatano, huku jumla ya vifo vilivyotokea juzi vilikuwa 981, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kutokea tangu mwezi Aprili.

Aina mpya ya virusi siyo tu kwamba inaenea kwa kasi mjini London na viunga vyake, lakini sasa inaripotiwa katika sehemu za kati na kaskazini magharibi mwa Uingereza.

Katika mkutano na wanahabari hapo juzi waziri mkuu Boris Johnson aliwataka watu kuwa na uelewa wa sheria hizo kali, akitaja kasi kubwa ambayo virusi vinaenea.

Katika hatua nyengine Uingereza imeidhisha chanjo ya corona ya Oxford na AstraZeneca, ikiwa nchi ya kwanza duniani kuidhinisha chanjo hiyo.

Mamlaka za Uingereza tayari zimekuwa zikiwachanja watu kwa chanjo iliyotengenezwa na kampuni kubwa ya kutengeneza dawa ya Marekani ya Pfizer na ile ya BioNTech ya Ujerumani.